Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Adam Kighoma Malima, amesema wananchi wa mkoa huo wanasubiri kwa hamu kuanza kwa Mradi wa Kuchakata Gesi Asilia (LNG), wakitarajia kuwa mradi huo utachochea ukuaji wa uchumi, kuongeza fursa za ajira na kuleta maendeleo makubwa kwa wananchi.

Mhe. Malima ameyasema hayo leo, Oktoba 26, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Likong’o, iliyozinduliwa na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, akiwa Mgeni Rasmi.

Mhe. Malima ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua zinazochukuliwa kuhakikisha maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo yanaendelea, baada ya wananchi kusubiri kwa zaidi ya miaka 15.

Aidha, Mhe. Malima ameipongeza Wizara ya Nishati na taasisi zake kwa juhudi za kuhakikisha majadiliano na maandalizi yanayohusu mradi huo yanakamilishwa, akieleza kuwa Mkoa wa Lindi una matarajio makubwa ya kunufaika na fursa zitakazotokana na uwekezaji huo.

Akizungumzia umuhimu wa elimu katika maandalizi ya mradi huo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema ni muhimu kuwekeza katika elimu na kuwaandaa vijana wenye ujuzi utakaowawezesha kushiriki katika fursa za ajira na shughuli za kiuchumi zitakazotokana na mradi wa LNG.

Ameeleza kuwa wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Awali na Msingi ya Likong’o ni miongoni mwa kizazi kinachotarajiwa kunufaika na fursa hizo katika siku zijazo, hivyo akasisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu na maandalizi ya rasilimali watu katika mkoa huo.