Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amekutana na kuzungumza na wananchi wa Msalala, mkoani Shinyanga, waliomsubiri hadi usiku wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kahama–Bulyanhulu Junction–Kakola yenye urefu wa kilomita 73.

Wananchi hao walijitokeza kumsubiri Waziri huyo ili kupata ufafanuzi kuhusu hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa barabara hiyo pamoja na mikakati ya Serikali kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Akizungumza na wananchi hao, Waziri Kadogosa alisema tayari ametoa maelekezo kwa mkandarasi kuhakikisha ujenzi wa mradi huo unakamilika kwa mujibu wa muda uliowekwa katika mkataba na kusisitiza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2026.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya barabara na haitasita kuchukua hatua dhidi ya wakandarasi watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba.

Kadogosa aliongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya usafiri, kuunganisha maeneo mbalimbali na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii.

Alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za miundombinu.

Sambamba na hilo, Waziri Kadogosa alisema kuwa Serikali itajenga barabara ya Bulyanhulu–Mtakuja Junction yenye urefu wa kilomita 68 kwa kiwango cha lami.

Alifafanua kuwa ujenzi wa barabara hiyo utasaidia kupunguza umbali wa safari kati ya Shinyanga na Geita, kurahisisha mawasiliano na kuimarisha shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo.

Kwa upande wao, Mbunge wa Msalala, Mhe. Mabula Magangila, na Mbunge wa Kahama Mjini, Mhe. Benjamin Ngayiwa, wamesema wananchi wanatarajia kuona barabara hiyo ikikamilika kwa wakati kutokana na umuhimu wake katika kukuza shughuli za kiuchumi na kuchochea maendeleo ya mkoa wa Shinyanga.

Vilevile, viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa wa barabara hiyo kuwekwa taa ili kuimarisha usalama na kurahisisha usafiri kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo.