Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, CPSP Hassan Rugwa, amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa utoaji elimu kwa umma kuhusu Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la Afrika Mashariki, ili kujenga uelewa na kutoa maoni yatakayochangia mustakabali wa mtangamano wa kikanda.
Ametoa wito huo alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, katika ufunguzi wa zoezi la kitaifa la utoaji elimu kwa umma kuhusu Rasimu hiyo, lililofanyika mkoani Kigoma, Oktoba 26, 2026.
Bw. Rugwa amesisitiza umuhimu wa wananchi kuelewa madhumuni ya Fungamano la Kisiasa na kutumia fursa hiyo kutoa maoni yenye tija, huku akiyahimiza makundi mbalimbali ya jamii, wakiwemo wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na wafanyabiashara kushiriki kikamilifu.
Akiwasilisha mada kuhusu Fungamano la Kisiasa la Afrika Mashariki Bw. Salehe Mubarak ambae ni mjumbe wa Kamati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Uandishi wa Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la Afrika Mashariki ameeleza kuwa mchakato huo ni hatua ya mpito kuelekea Shirikisho la Kisiasa, iliyopitishwa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka 2017, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kikanda hatua kwa hatua.
Amefafanua kuwa Fungamano la Kisiasa halimaanishi nchi wanachama kupoteza uhuru na mamlaka yao ya kitaifa, bali ni mfumo unaowezesha nchi kushirikiana kwa karibu katika maeneo ya kimkakati kwa manufaa ya wananchi.
Amebainisha maeneo muhimu yanayohitaji maoni ya wananchi kuwa ni pamoja na muundo wa utawala, mfumo wa kufanya maamuzi, maeneo ya ushirikiano, uhusiano kati ya serikali za nchi wanachama na mamlaka ya Fungamano, pamoja na namna ya kugharamia shughuli zake.
Katika hatua nyingine, washiriki wa zoezi hilo wamepata fursa ya kufanya majadiliano, kuuliza maswali na kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Fungamano la Kisiasa, hatua iliyowasaidia kuongeza uelewa na kutoa mitazamo yao kuhusu mustakabali wa mtangamano wa Afrika Mashariki.
Zoezi hili ni sehem ya Juhudi za Serikali na Jamhuri ya Muungano kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika Maandalizi ya Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa, ili kujenga Mtangamano unaozingatia Maslahi matarajio na maoni ya Wananchi.

