Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema mkakati wa serikali ni kuboresha reli ya zamani (MGR) kwa kuweka mataruma ya zege, hatua itakayosaidia kuongeza mzigo kutoka tani 500,000 hadi milioni 18 kwa mwaka.

Pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga Sh bilioni 379 kwa ajili ya kuboresha reli ya zamani (MGR), kipande cha Kaliua–Mpanda, pamoja na kujenga kiwanda cha kuzalisha mataruma ya zege.

Akizungumza baada ya kutembelea kiwanda hicho, Profesa Mbarawa alisema maboresho hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza uwezo wa reli kusafirisha mizigo kwa kubadilisha mataruma ya chuma na kuweka ya zege na kuondoa utegemezi wa barabra katika kusafirisha mizigo.

Aidha, Profesa Mbarawa alisema ujenzi wa kiwanda hicho utapunguza gharama za uzalishaji wa mataruma na kurahisisha uboreshaji wa reli ya kati.

Alifafanua kuwa taruma moja la chuma linagharimu Sh 360,000, wakati taruma la zege linagharimu takribani dola 65, sawa na Sh 130,000.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Machibya Shiwa, alisema mataruma ya zege yana uzito wa kilogramu 250, ikilinganishwa na kilogramu 39.7 za mataruma yaliyopo, hali inayosaidia kuimarisha njia na kuruhusu treni kuongeza kasi.

Katika hatua nyingine, Shiwa alisema Waziri Mbarawa amemuagiza mkandarasi wa kipande cha tatu cha reli ya kisasa (SGR), eneo la bonde la Nyahua lenye urefu wa kilometa 100, kuongeza kasi ya kazi.

Alisema TRC inatarajia huduma za SGR kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kuanza mwaka 2028.

Uboreshaji huo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji, kupunguza gharama za biashara na kuchochea maendeleo ya uchumi nchini.