NA SOPHIA KINGIMALI, DAR ES SALAAM

HUDUMA za maktaba nchini zinatarajiwa kuimarika kufuatia maboresho ya Sheria ya Huduma za Maktaba Tanzania, Na. 102, iliyotolewa Oktoba 2, mwaka huu, ambayo imepanua wigo wa huduma hizo na kuweka viwango vinavyopaswa kuzingatiwa na waendeshaji wa maktaba.

Maboresho hayo yanatarajiwa kuimarisha usimamizi wa maktaba na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaendana na mahitaji ya jamii, huku hatua inayofuata ikiwa ni kuandaa kanuni zitakazowezesha utekelezaji wa sheria hiyo.

Akizungumza leo Octoba 22,2026 Jijini Dar es salaam ikiwa ni siku ya mwisho ya Kongamano la Nne la Huduma za Maktaba Tanzania, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania,(TLSB) Mboni Ruzegea, amesema sheria hiyo imeainisha makundi mbalimbali yanayolengwa na huduma za maktaba pamoja na kuweka viwango vya uendeshaji wa huduma hizo nchini.

Amesema maandalizi ya kanuni hizo yanahitaji ushiriki wa wakutubi, waendesha maktaba na wadau wa huduma za nyaraka ili kuhakikisha maoni yao yanazingatiwa na kuwezesha utekelezaji wenye tija.

Ametoa wito kwa wadau hao kushiriki katika vikao vitakavyoitishwa hivi karibuni kwa ajili ya kujadili maeneo mbalimbali ya kanuni hizo, akisisitiza kuwa uelewa wa pamoja ni muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma.

Ruzegea amesema kongamano hilo pia limejadili namna maktaba zinavyoweza kutumia teknolojia za kisasa, ikiwamo akili unde (AI), kuboresha huduma na kuendana na mabadiliko ya mahitaji ya watumiaji katika zama za kidijitali.

Amesema siku ya kwanza ya kongamano hilo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alizindua mfumo wa maktaba mtandao wa taifa unaolenga kuwahudumia wadau mbalimbali, wakiwamo wachapishaji, waandishi, taasisi, vyuo, shule na wananchi.

Ameongeza kuwa wadau wamejadili pia umuhimu wa kuboresha mitaala ya taaluma ya ukutubi ili iendane na maendeleo ya teknolojia, pamoja na dhana ya embedded librarianship iliyowasilishwa na Profesa Mwantimwa.

Aidha Ruzegea amesema kuwa, kongamano hilo limejadili pia namna ya kuimarisha Chuo cha SLADS ili kuboresha kozi zinazotolewa na kuhakikisha mafunzo yanakidhi mahitaji ya sasa ya taaluma ya ukutubi na sayansi ya taarifa.

Ametaja mada nyingine zilizojadiliwa kuwa ni mapambano dhidi ya rushwa na taratibu za manunuzi ya umma katika mazingira ya kiteknolojia, akisema mada hizo zina umuhimu katika kuimarisha weledi na uwajibikaji katika taasisi.

Amewahimiza wananchi, hususan vijana, kutumia maktaba kama maeneo ya kujifunza, kubadilishana mawazo na kushirikiana katika shughuli za maendeleo, badala ya kuzichukulia kuwa sehemu za kusoma vitabu pekee.

Katika hatua nyingine, Profesa Evans Mwema, Profesa wa Usimamizi wa Taarifa na Teknolojia ya Habari kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema matumizi ya AI yanapaswa kujumuishwa katika mitaala ya ukutubi na sayansi ya taarifa ili kuwajengea wakutubi uwezo wa kutumia teknolojia hiyo katika majukumu yao.

Amesema kuingiza elimu ya AI katika mitaala hiyo kutasaidia kuboresha utendaji wa wakutubi na kuimarisha usomaji, sambamba na kuziandaa huduma za maktaba kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050