Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Saidi Yakubu, tarehe 21 Oktoba 2026 amekutana na Uongozi wa Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), ukiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, Dkt. Mwamini Tulli, na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Eliamani Sedoyeka, ukiwa jijini Paris karika jitihada za kukuza ushirikiano wa taasisi hiyo na wadau wengine duniani.

Kikao hicho kimehusu kuendeleza ushirikiano wa kimkakati kati ya IAA na taasisi za Ufaransa, pamoja na nafasi ya Ubalozi katika kuwezesha mahusiano hayo na kupanua fursa za elimu, mafunzo na utafiti.

Wakiwa Paris, viongozi hao wa IAA pia watakutana na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO pamoja na wadau wengine muhimu, kwa lengo la kujadili fursa za ushirikiano na kuimarisha mahusiano ya kitaasisi.

Ushirikiano huo unalenga kuimarisha ubadilishanaji wa maarifa na uzoefu, kukuza uwezo wa kitaaluma na kuendeleza ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira, kwa manufaa ya wanafunzi na wahadhiri wa IAA.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za IAA kupanua ushirikiano wa kimataifa, huku Ubalozi ukiendelea kuwa kiungo kati ya taasisi za Tanzania na washirika wa Ufaransa pamoja na mashirika ya kimataifa katika kuendeleza elimu na rasilimali watu.