*******************
19,Juni
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
JESHI la polisi mkoani Pwani,linawashikilia wahamiaji haramu sita ambao ni raia kutoka nchini Ethiopia kwa kosa lakuingia nchini bila kibali,”:huku likikamata watu wengine 29 kwa kujihusisha na matukio ya uvunjaji nyumba usiku na kuiba.
Watuhumiwa hao wamekamatwa kufuatia msako mkali na oparesheni dhidi ya vikundi vya vijana wa mitaani wanaojihusisha na wizi kwa kuvunja,kupora na kukaba raia wema huko wilaya ya kipolisi Chalinze .
Akielezea kuhusiana na matukio hayo,kamanda wa polisi mkoani Pwani,Wankyo Nyigesa alisema,baadhi yao walikamatwa wakiwa na mali kadhaa,madawa ya kulevya aina ya bangi kete 142,puli nne,pombe haramu ya moshi lita 25 na pikipiki moja.
Anabainisha kwamba,pia kumekamatwa magunia 90 ya mkaa uliovunwa bila uhalali ,mashuka,raba,vitenge,mafuta ya pikipiki na mafuta ya kula yanayodaiwa kuingizwa kwa kukwepa ushuru lita 300.
Akizungumzia kuhusu wahamiaji haramu alisema ,watafikishwa katika idara ya uhamiaji kwa taratibu nyingine za kisheria.
Kamanda huyo alitoa rai kwa jamii ,kuwa itambue uhalifu haulipi na hauna faida kwani siku za mwizi ni arobaini na akishikwa mtu akijihusisha na uhalifu atakiona.
Vilevile anawataka walioibiwa kufika katika kituo cha polisi Chalinze kutambua mali zao .