Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa mazingira Kahama-Shinyanga (KASHWASA) imetakiwa kuandaa andiko kuweza kufadhiliwa na taasisi za fedha ili kuongeza uzalishaji wa maji katika chanzo cha Ihelela. 

Naibu wa Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Kundo Andrea Mathew (Mb) amesema hayo katika kikao na watendaji wa Sekta ya Maji wa mkoa wa Shinyanga kabla ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji.

“Niwaagize KASHWASA muandae andiko, linapaswa kubainisha gharama za uwekezaji, gharama za uendeshaji na matengenezo, mpango wa utekelezaji, mahitaji ya fedha, vyanzo vinavyopendekezwa vya ufadhili, pamoja na makadirio ya mapato na matumizi” Mhandisi Kundo amesema.

Amesisitiza kuwa uchambuzi wa kifedha unapaswa kuonyesha uwezo wa KASHWASA kurejesha fedha, mtiririko wa fedha, muda wa kurejesha uwekezaji, na kiwango cha faida.

Ameainisha kuwa andiko linapaswa kuonesha tathmini ya mahitaji ya maji kwa sasa na kwa miaka ijayo, mpango wa mauzo na usambazaji wa maji, mikakati ya kuongeza makusanyo, pamoja na makubaliano ya ununuzi wa maji kutoka kwa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira. Pia, liainishe dhamana au mifumo ya kuhakikisha ulipaji wa fedha, ikiwemo mikataba ya muda mrefu ya ununuzi wa maji, makubaliano ya ulipaji, na mifumo ya ufuatiliaji wa mapato.