Meneja wa Shule hiyo , Mchg. Manase Meshorori akizungumza katika mahafali hayo jijini Arusha
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo ,Mary Mollel akizungumza katika.mahafali hayo
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha .WAZAZI na walezi wametakiwa kutowaharakisha watoto kuingia katika mambo ya utu uzima kabla ya kufikia umri unaostahili, badala yake wasisitiziwe umuhimu wa malezi yanayozingatia hatua za ukuaji wa mtoto katika kipindi hiki cha utandawazi.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Mchungaji mwenza wa usharika wa Engarenarok Mchg. Zakayo Loibooki kwa niaba ya Mchungaji kiongozi wa usharika huo ,Mchungaji Jasson Kahembe katika mahafali ya 18 ya darasa la saba katika shule ya awali na msingi ya Kimandolu Lutheran iliyopo jijini Arusha ambapo jumla ya wanafunzi 29 wamehitimu masomo yao.
Amesema wazazi wanapaswa kuimarisha malezi yanayozingatia misingi ya Kikristo na maadili mema ili kuwajengea watoto msingi imara wa maisha.
Mchg. Loibooki amewakumbusha wazazi umuhimu wa kumlea mtoto katika njia impasayo ili aendelee kuzingatia mafundisho hayo hata anapokuwa mtu mzima.
“Watoto hujifunza kwa kiasi kikubwa kupitia tabia na mwenendo wa watu wazima wanaowazunguka, hivyo wazazi wanapaswa kuwa mifano bora katika mazungumzo, matendo na namna wanavyoishi.”amesema Mchg Loibooki.
Ameongeza kuwa baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika jamii zinaweza kuzuiwa ikiwa watu wazima watatimiza wajibu wao wa kuwalea watoto katika misingi sahihi ya maadili.
Aidha, amewataka wazazi, walimu na walezi kushirikiana katika kuwafundisha watoto mambo yanayolingana na umri wao, huku wakiepuka kuwapa mafunzo au majukumu ya utu uzima kabla ya wakati.
Aidha amewataka wanafunzi waliohitimu, kuendeleza nidhamu, heshima na maadili waliyojifunza shuleni wanapojiandaa kuendelea na elimu ya sekondari huku akiwataka kuchagua kwa makini tabia za kuiga katika mazingira mapya watakayokutana nayo.
Naye Meneja wa Shule hiyo , Mchg. Manase Meshorori, amesema shule hiyo imeendelea kufanya vizuri kitaaluma kutokana na juhudi za walimu katika kutoa elimu bora pamoja na kuwalea wanafunzi katika misingi ya maadili mema na uzalendo.
Meshorori amesema shule hiyo inajivunia matokeo ya mwaka 2025, ambapo wanafunzi wote 30 waliofanya mtihani walifaulu, huku 24 wakipata daraja A na sita wakipata daraja B.
Amesema matokeo hayo ni ishara ya maendeleo ya shule hiyo katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu yenye ubora, inayowawezesha kujiandaa kwa hatua nyingine za masomo na maisha yao ya baadaye.
Meshorori ameongeza kuwa elimu inayotolewa shuleni hapo inaambatana na malezi ya kimaadili yanayolenga kuwajenga watoto kuwa watu wenye nidhamu, uwajibikaji na uzalendo, ili waweze kulitumikia taifa na kuchangia maendeleo ya jamii.
Aidha, amewahimiza wazazi na walezi kuchagua shule bora kwa ajili ya watoto wao, akiwakaribisha kujiunga na Kimandolu Lutheran ili kupata huduma za elimu zinazolenga kuwaandaa watoto kuwa na msingi imara wa maisha ya baadaye.
“Shule yetu inawakaribisha wazazi bila masharti magumu ya udahili,hivyo nawaomba muwalete watoto wenu ili washirikiane na walimu katika kuwalea, kuwafundisha na kuwaandaa kuwa raia wenye manufaa kwa Taifa.”amesema Meshorori.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo ,Mary Mollel, amesema shule hiyo imeweka kipaumbele katika kutoa elimu bora inayoambatana na malezi ya kidini na maadili mema, ili kuwajenga wanafunzi kuwa na hofu ya Mungu, nidhamu na tabia njema katika jamii.
Mollel amesema shule hiyo inaendesha vipindi vya dini mara tatu kwa wiki pamoja na siku mbili za gwaride, hatua inayolenga kuwajenga wanafunzi katika misingi ya maadili na uwajibikaji.
Amesema tangu kuanza kwa shule hiyo hadi sasa hivi imekuwa ikiendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kujivunia ufaulu wa asilimia 100 kwa miaka yote tangu kuanzishwa kwa shule hiyo.

