Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema ziara zake nchini Qatar, Hispania na Armenia zimefungua fursa muhimu za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika uwekezaji, michezo na uhifadhi wa mazingira, hatua inayotarajiwa kuchangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 18 Oktoba 2026, alipozungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, baada ya kurejea nchini kutoka ziara hizo.

Akizungumzia ziara yake nchini Qatar, Rais Dkt. Mwinyi amesema alikutana na uongozi wa kampuni ya Alfardan, inayojihusisha na ujenzi wa hoteli, majengo ya makaazi na miradi mingine ya maendeleo, ambapo kampuni hiyo imeonesha nia ya kuwekeza Zanzibar.

Amesema hatua hiyo inatarajiwa kuchangia ukuaji wa sekta ya utalii, kuongeza ajira na biashara pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi. Rais Dkt. Mwinyi amewakaribisha wawekezaji hao kutoka Qatar na mataifa mengine kuja Zanzibar, huku Serikali ikiendelea kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji kwa mitaji ya ndani na nje.

Akizungumzia ziara yake nchini Hispania, Rais Dkt. Mwinyi amesema alitembelea Real Madrid Foundation ambako alishuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Real Madrid Foundation na Unicorn Zanzibar Sports Limited, yenye lengo la kukuza na kuendeleza vipaji vya soka kwa vijana wa Zanzibar.
Amesema kupitia ushirikiano huo, makocha wenye uzoefu kutoka Real Madrid Foundation wanatarajiwa kuja Zanzibar kutoa mafunzo kwa vijana wenye vipaji, sambamba na kuwajengea uwezo makocha wa ndani pamoja na kuendeleza wachezaji chipukizi.

Rais Dkt. Mwinyi amesema hatua inayofuata ni kuanzishwa kwa Real Madrid Academy ya Zanzibar, itakayowezesha vijana kupata mafunzo ya soka kwa mfumo maalumu na kuongeza nafasi zao kushiriki mashindano pamoja na kupata fursa katika klabu mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Amesema ushirikiano huo unaenda sambamba na uwekezaji wa Serikali katika miundombinu ya michezo, ikiwemo viwanja vya mpira vya Amaan Complex, Mao na Fumba, ambapo hatua inayofuata ni kuhakikisha miundombinu hiyo inaambatana na mafunzo bora, makocha wenye uwezo na programu madhubuti za kukuza vipaji.

Rais Dkt. Mwinyi ameitaka Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo kuhakikisha makocha wa Zanzibar wanapata elimu na mafunzo bora, ikiwemo fursa za kwenda nje ya nchi kujifunza mbinu za kisasa za ufundishaji na ukuzaji wa vipaji.

Akizungumzia ziara yake nchini Armenia, Rais Dkt. Mwinyi amesema alipata fursa ya kushiriki majadiliano na viongozi wa mataifa mbalimbali kuhusu mazingira, uhifadhi wa rasilimali za asili na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema Zanzibar inakabiliwa na changamoto za kimazingira, zikiwemo mmomonyoko wa fukwe, kuingia kwa maji ya chumvi katika visima na kupungua kwa upatikanaji wa maji, hali inayohitaji kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimataifa katika kutafuta suluhisho endelevu.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Tanzania ina rasilimali muhimu za mazingira, ikiwemo misitu, wanyamapori na maeneo ya bahari, hivyo juhudi za kuzihifadhi zinapaswa kwenda sambamba na kuhakikisha wananchi wanaozitegemea wanaendelea kunufaika kupitia matumizi endelevu ya rasilimali hizo.

Aidha, amesema katika sekta ya uvuvi ni muhimu kuendelea kuweka maeneo maalumu ya uhifadhi wa bahari, hususan kulinda mazalia ya samaki na kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinaendelea kupatikana kwa manufaa ya wananchi na vizazi vijavyo.

Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa mafanikio ya ziara hizo yatategemea utekelezaji wa masuala yaliyojadiliwa na makubaliano yaliyofikiwa, ili ushirikiano ulioanzishwa katika uwekezaji, michezo na uhifadhi wa mazingira ulete matokeo yanayoonekana kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, walihudhuria viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Chama Cha Mapinduzi.

Rais Dkt. Mwinyi aliondoka nchini tarehe 7 Oktoba 2026, katika ziara zilizompeleka Qatar, Hispania na Armenia kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika uwekezaji, michezo na uhifadhi wa mazingira.