📌 Asema uwanja huo utarahisisha usafiri, kuvutia uwekezaji na kukuza utalii.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Iringa utafungua fursa za kiuchumi, kuvutia uwekezaji na kurahisisha usafiri kwa wananchi, wafanyabiashara na watalii.

Mhe. Ndejembi ameyasema hayo mkoani Iringa alipokagua maendeleo ya awamu ya pili ya mradi huo inayohusisha ujenzi wa jengo la abiria na maegesho ya magari, akieleza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania.

Amesema miundombinu bora ya usafiri wa anga itapanua fursa za biashara na uwekezaji, huku akiwataka viongozi na watendaji wa Serikali kusimamia kwa uadilifu fedha za umma, kupambana na rushwa na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa uwanja huo, iliyohusisha barabara ya kuruka na kutua ndege (runway), barabara za maingilio ya ndege (taxiways) na jengo la huduma za umeme (powerhouse), imekamilika kwa asilimia 100 kwa gharama ya Shilingi bilioni 68.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kujenga barabara ya Iringa–Msembe yenye urefu wa kilomita 140, inayounganisha mkoa huo na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa lengo la kukuza utalii. Aidha, ameishukuru Serikali kwa kutenga zaidi ya Shilingi bilioni 300 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya ujenzi mkoani Iringa.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema ujenzi wa jengo la abiria na maegesho ya magari umefikia asilimia 49 na unagharimu Shilingi bilioni 41.