Dar es Salaam

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera amesema zoezi la uchimbaji wa visima vitatu vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay mkoani Mtwara limekamilika kwa mafanikio makubwa, ambapo imegunduliwa gesi asilia inayotarajiwa kuongeza kiasi cha nishati hiyo kutoka futi za ujazo trilioni 57.54 zilizopo sasa.

Amesema Serikali inatarajia kuzindua visima hivyo wiki ijayo katika Kijiji cha Msimbati mkoani Mtwara, ambapo pia itatangaza kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa kutokana na shughuli hizo za uchimbaji.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 18, 2026, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, Mhe. Homera amesema visima hivyo, viwili vya uendelezaji na kimoja cha utafiti, vimechimbwa kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na mwekezaji, kampuni ya M&P.

Amesema ugunduzi huo unazidi kuiwezesha Serikali kuwa na nishati ya gesi asilia kwa ajili ya kukidhi mahitaji mbalimbali ya nchi pamoja na kufungua fursa zaidi za uwekezaji katika sekta hiyo.

Mhe. Homera ameongeza kuwa Serikali kupitia TPDC inaendelea na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Eyasi-Wembere, Lindi-Mtwara, Songo Songo Magharibi, Mnazi Bay Kaskazini na Ntorya.

Ameeleza kuwa shughuli za uchukuaji wa data za mitetemo zinaendelea katika vitalu vya Eyasi-Wembere na Lindi-Mtwara na zinatarajiwa kukamilika Desemba 2026, huku maandalizi ya uchorongaji wa kisima cha uzalishaji na usimikaji wa mitambo ya kusafisha gesi yakiendelea katika Kitalu cha Ntorya.

Kuhusu maendeleo ya Kitalu cha Ntorya, Mhe. Homera amesema ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi lenye urefu wa kilomita 35 kutoka Ntorya hadi Madimba umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026, huku uzalishaji wa gesi ukitarajiwa kuanza mapema mwaka 2027 na kufikia futi za ujazo milioni 40 kwa siku.

Ameeleza kuwa TPDC inaendelea kushirikiana na kampuni binafsi katika usambazaji wa gesi asilia majumbani na kwenye magari (CNG), ambapo hadi Septemba 2026, jumla ya vituo 22 vilikuwa vimekamilika na kuanza kutoa huduma.

Katika hatua nyingine, Homera amesema wiki ijayo Serikali inatarajia kusaini na kukabidhi leseni mpya za utafutaji mafuta na gesi asilia (PSA) kwa TPDC, hatua itakayoliwezesha shirika hilo kuendelea na shughuli za utafutaji, uzalishaji na uendelezaji wa rasilimali hizo nchini ambapo Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi atakuwa mgeni rasmi.

Akizungumzia sekta ya umeme, Mhe. Homera amesema uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini umeongezeka na kufikia Megawati 4,646 kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwemo maji, gesi asilia, jua na nishati nyingine mbadala, huku Serikali ikiendelea kutekeleza mkakati wa kuongeza uwezo huo hadi Megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.

Amesema katika kuimarisha uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati jadidifu, Serikali imekamilisha Mradi wa Kishapu I wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 50 za umeme wa jua, huku ujenzi wa Kishapu II wenye uwezo wa Megawati 100 ukiendelea.

 Aidha, miradi mingine yenye uwezo wa zaidi ya Megawati 600 ipo katika hatua mbalimbali za majadiliano na upembuzi.

Kuhusu miundombinu ya usafirishaji umeme, Waziri huyo amesema Serikali imekamilisha Mradi wa Chalinze–Dodoma tangu Septemba 2026, ambao umeimarisha ubora na kiwango cha umeme kinachofika katika mikoa ya Magharibi na Kaskazini mwa nchi.

Ameongeza kuwa Mradi wa Iringa–Tunduma–Sumbawanga unatarajiwa kuwashwa Novemba 2026 na kuunganisha Mkoa wa Rukwa katika Gridi ya Taifa kwa mara ya kwanza, huku Mradi wa Chalinze–Kinyerezi–Mkuranga ukitarajiwa kuwashwa Februari 2027 ili kuimarisha upatikanaji wa umeme jijini Dar es Salaam na maeneo ya viwanda ya Mkuranga.

Aidha, amesema utekelezaji wa Mradi wa Songea–Tunduru–Masasi–Maumbika unaendelea kwa kasi, ukiwa na lengo la kuunganisha mikoa ya Lindi na Mtwara katika Gridi ya Taifa na kuondoa changamoto za upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo.