Afisa mahusiano wa Swisscontact Masunga Isumbi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu namna wanavyotoa mafunzo kwa vijana na wanavyonufaika.
Faudhia Balthazar akieleza namna alivyonufaika na mradi huo
Na ,Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa :Kwa vijana wengi wa vijijini waliokuwa wamekata tamaa, elimu ndogo na umasikini mkubwa vilikuwa vikwazo vya kutopita. Lakini kwa miaka minne sasa, kupitia Mradi wa Skills for Employment Tanzania (SET) Awamu ya Pili, maisha yao yamebadilika kabisa. Ujuzi wa mikono umekuwa ufunguo wa ajira, kipato na matumaini mapya.
Mradi huo, unaofadhiliwa na Shirika la Uswisi la Maendeleo na Ushirikiano (SDC) kupitia Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na kutekelezwa na Swisscontact, umefanya kazi kuanzia katikati ya 2022 hadi katikati ya 2026 katika mikoa ya Rukwa , Morogoro na Iringa.
SET iliwalenga vijana walio katika mazingira hatarishi zaidi wenye umri wa miaka 15 hadi 24, hususan vijana wa kike . Wengi wao wanaishi chini ya mstari wa umasikini wa kimataifa, wana elimu ndogo, hawana ajira au wana ajira hatarishi, na wanashindwa kupata mitaji.
Lengo lilikuwa moja tu kuwapa ujuzi unaoendana na soko la ajira ili wapate kipato cha uhakika.
Mradi ulifanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais – TAMISEMI pamoja na wadau wa umma na binafsi wa elimu ya ufundi stadi (VSD) na ujasiriamali. Kama mwezeshaji, SET ilikamilisha juhudi za Serikali za kuwawezesha vijana kiuchumi.
Kiini cha SET kilikuwa programu za VSD zisizo rasmi, za vitendo, zenye wastani wa miezi sita. Kabla ya kuanza mafunzo, mradi ulifanya tafiti za soko la ajira ili kuhakikisha fani zinazofundishwa zinaendana na fursa halisi za kiuchumi katika jamii husika.
Afisa mahusiano wa Swisscontact Masunga Isumbi akizungumza na waandishi wa habari katika mabanda ya maonesho yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Ndua Manispaa ya Sumbawanga anasema mafunzo yanajumuisha fani mbalimbali kama ufugaji kuku, kusindika chakula, kilimo cha bustani (horticulture), agroforestry, uzalishaji wa mazao, ufundi, ushonaji na biashara.
“Lakini SET haikuwafundisha vijana tu. Iliimarisha pia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) na watoa mafunzo wengine wa ndani.”amesema Isumbi
Kupitia Maendeleo Endelevu ya Kitaaluma (CPD), walimu waliboresha mbinu za kufundisha na kutengeneza mazingira jumuishi ya kujifunza, ili mifumo iendelee hata baada ya mradi kuisha.
Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Nicole Providoli, anasema SET ni mfano wa jinsi maendeleo ya kweli yanavyopaswa kufanyika.
“SET inaonyesha kuwa maisha endelevu yanahitaji zaidi ya mafunzo pekee – yanahitaji mifumo inayowafanyia kazi vijana. Uswisi imekuwa ikiunga mkono Tanzania tangu miaka ya 1960, na inaendelea kuhakikisha hakuna kijana anayeachwa nyuma.”
Miongoni mwa walionufaika ni Faudhia Balthazar Baada ya kupata mafunzo ya kusindika chakula, aliweza kuanzisha biashara yake mwenyewe, kujiunga na kikundi cha kuweka na kukopa, na sasa anasaidia familia yake.
“Sasa hakuna kurudi nyuma. Ujuzi nilioupata umenibadilisha. Naweza kuendesha biashara yangu, kupata kipato na kusimamia maisha yangu,” anasema Faudhia.
Vijana wengine walitumia akiba waliyoipata kupitia kilimo cha bustani kununua mifugo. Hatua kwa hatua, kilimo kidogo kikawa chanzo cha kipato kikubwa, na akiba ikaanza kujenga mali ya kudumu.
Kupitia mfumo wa kidijitali wa ufuatiliaji, SET iliweza kufuatilia safari ya kila kijana kuanzia kujiunga hadi kupata ajira. Matokeo yanaonyesha mabadiliko makubwa ongezeko la vijana wenye ajira, kipato na ujasiri wa kuendesha biashara zao wenyewe.
