NA DENIS MLOWE IRINGA 

MBUNGE wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, amewaleta wadau wa maendeleo kutoka Canada katika Kituo cha Afya Mgama, wilayani Iringa, kwa lengo la kutafuta namna ya kusaidia kukamilisha ujenzi wa wodi iliyodumu kwa takribani miaka 11 bila kukamilika, pamoja na kutafuta suluhisho la changamoto ya usafiri wa wagonjwa.

Kiswaga amesema wageni hao wanatoka katika kampuni ya Clear 8, inayojihusisha na teknolojia za maji, ambao wameonyesha nia ya kushirikiana katika kusaidia huduma za maji na afya katika Jimbo la Kalenga.

Amesema ameamua kuwapeleka katika Kituo cha Afya Mgama ili wajionee hali halisi ya miradi ya maendeleo inayohitaji msaada, hususan wodi iliyojengwa kwa nguvu za wananchi lakini bado haijakamilika tangu kuanzishwa kwake.

Amesema ziara hiyo inalenga kuwawezesha wadau hao kutathmini changamoto zilizopo na kuona maeneo ambayo wanaweza kushirikiana na wananchi katika kuboresha huduma za afya.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mgama, Job Mbwilo, amemshukuru mbunge huyo kwa kuwaunganisha na wageni hao, akisema ana matumaini ziara hiyo itasaidia kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikisumbua wananchi kwa muda mrefu.

Mbwilo amesema ujenzi wa wodi hiyo ulianza Februari mwaka 2015, lakini hadi sasa haujakamilika, licha ya wananchi kuendelea kujichangisha ili kukamilisha ujenzi huo na kuiwezesha jamii kupata huduma bora za afya.

Amesema kukamilika kwa wodi hiyo kutasaidia kupunguza changamoto za utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa kata hiyo na maeneo jirani.

Aidha, diwani huyo amesema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ya usafiri wa wagonjwa, hususan ukosefu wa ambulansi ya kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji kupelekwa katika vituo vingine vya afya kwa matibabu zaidi.

Ameeleza kuwa changamoto hiyo imekuwa ikiathiri upatikanaji wa huduma za haraka kwa wagonjwa, akitoa matumaini kuwa kupitia ushirikiano na wadau hao, kituo hicho kinaweza kupata msaada wa ambulansi na kukamilisha wodi hiyo.

Mbwilo amewashukuru wadau hao kwa kutembelea kituo hicho na kuonesha nia ya kuona namna ya kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, huku akiwakaribisha kuendelea kushirikiana na jamii ya Mgama katika shughuli za maendeleo.