Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, amewapongeza Watanzania waishio ughaibuni kwa uzalendo wao na kuwahimiza kuendelea kuwekeza nyumbani, wakitumia elimu, ujuzi, uzoefu na mitandao yao kuchangia maendeleo ya taifa.

Mhe. Kombo ameyasema hayo tarehe 17 Oktoba 2026 alipojiunga kwa njia ya simu katika hafla ya Watanzania waishio Ufaransa, iliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini humo kwa lengo la kufahamiana, kuimarisha mshikamano na kufurahi pamoja.

Amewapongeza kwa ushirikiano wao na Serikali na Ubalozi, hususan katika kufanikisha maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani na Kongamano la Pili la Kimataifa la Lugha ya Kiswahili yaliyofanyika Paris mwezi Julai mwaka huu.

Aidha, amewahimiza kujisajili kupitia mfumo wa Diaspora Digital Hub na kueleza kuwa Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala la Hadhi Maalumu kwa Diaspora kwa kuzingatia maboresho yaliyoelekezwa na Bunge.

Waziri Kombo pia alisikiliza na kujibu maswali ya Watanzania hao, huku akipongeza Ubalozi kwa kuandaa hafla hiyo na kumwalika kuzungumza nao.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Saidi Yakubu, amesisitiza kuwa milango ya Ubalozi iko wazi kupokea maoni, mapendekezo na changamoto zao, na kuwahimiza kuendeleza umoja na ushirikiano katika kuitangaza Tanzania.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Watanzania kutoka maeneo mbalimbali ya Ufaransa, huku wengine wakijiunga kwa njia ya mtandao. Usiku huo ulipambwa na muziki na vyakula vya Kitanzania, ukiwa fursa ya kujuana, kujumuika na kuenzi utamaduni wa Tanzania.