Meneja wa TIRA Kanda ya Kaskazini, Dkt. Emmanuel Lupilya akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.
……………
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha .Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Kanda ya Kaskazini, imewataka wananchi, wafanyabiashara, wakulima na wadau wa sekta ya utalii kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa na mafuriko yanayoweza kuhusishwa na hali ya hewa ya El Nino , huku ikisisitiza umuhimu wa bima katika kupunguza hasara za kifedha.
Meneja wa TIRA Kanda ya Kaskazini, Dkt. Emmanuel Lupilya, amesema maandalizi ya mapema ni muhimu katika kulinda maisha, mali na vyanzo vya mapato ya wananchi, akiwataka kuchukua hatua za kinga badala ya kusubiri janga litokee ndipo waanze kutafuta suluhisho.
Amesema kupitia elimu kwa umma na ushirikishwaji wa wadau katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga, TIRA inaendelea kuhamasisha jamii kuelewa hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa na mafuriko, pamoja na namna ya kutumia huduma za bima kupunguza athari za kifedha zinazoweza kujitokeza.
Dkt. Lupilya amewahimiza wananchi kuhakikisha nyumba, biashara, magari, mazao, mifugo na mali nyingine zina bima inayolingana na mahitaji yao, akibainisha kuwa hatua hiyo inaweza kusaidia katika kurejesha hali ya kawaida baada ya kutokea kwa majanga yanayosababisha hasara zinazolipiwa na bima husika.
Aidha, amewataka wananchi kupitia na kuelewa masharti ya bima zao, ikiwemo hatari zinazolipiwa, vikwazo vilivyowekwa, taratibu za kuwasilisha madai na masharti ya malipo ya ada za bima ili kuepuka changamoto wakati wa kuhitaji huduma hizo.
Amesisitiza kuwa matumizi ya bima yanapaswa kwenda sambamba na hatua nyingine za kujikinga, ikiwemo kusafisha mifereji ya maji, kuimarisha usalama wa majengo na mali, kuepuka maeneo yanayokabiliwa na hatari ya mafuriko na kufuatilia taarifa rasmi za utabiri wa hali ya hewa.
Aidha Dkt. Lupilya amezitaka kampuni za bima, madalali na mawakala wa bima kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma zinazopatikana, huku akizihimiza mamlaka za serikali za mitaa na viongozi wa jamii kushirikiana katika kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na majanga.
“Ushirikiano kati ya wananchi na wadau mbalimbali ni muhimu katika kuongeza uelewa wa bima na kuwasaidia watu kufanya maamuzi sahihi kuhusu namna ya kulinda mali na shughuli zao za kiuchumi dhidi ya hatari zinazoweza kujitokeza.”amesema Dokta Lupilya .
Hata hivyo, amekumbusha kuwa bima haichukui nafasi ya hatua za kinga wala kufuata maelekezo ya usalama yanayotolewa na mamlaka husika, bali husaidia kupunguza athari za kifedha pale hasara inapotokea na kufunikwa na masharti ya bima husika.
Aidha ametoa wito kwa kila kaya, biashara na jamii kuanza maandalizi mapema kwa kulinda mali zao, kupata taarifa sahihi na kuchukua tahadhari zinazohitajika ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na El Nino.
“Usisubiri janga litokee ndipo uchukue hatua; jiandae sasa, linda kilicho muhimu kwako na tumia bima kujikinga dhidi ya hasara zisizotarajiwa,” ni ujumbe unaotolewa na TIRA kwa wananchi katika kuimarisha uelewa wa bima na ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga.
