Na Sophia Kingimali.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Nne la Kitaifa la Uboreshaji wa Huduma za Maktaba litakalofanyika Oktoba 20 hadi 22, mwaka huu, katika viwanja vya Maktaba Kuu ya Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dkt. Mboni Ruzegea, amesema kongamano hilo litajadili namna ya kuboresha huduma za maktaba kupitia mageuzi ya kidijitali, kwa lengo la kukuza maarifa na ujuzi kwa maendeleo endelevu. Amesema mkutano huo utawakutanisha wadau wa serikali na sekta binafsi, wachapishaji, waandishi, wasomaji na washirika wa maendeleo.

“Kaulimbiu yetu imejikita katika maboresho ya huduma za maktaba kupitia mageuzi ya kidijitali, kukuza maarifa na ujuzi kwa maendeleo endelevu,” alisema Dkt. Ruzegea wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya kongamano hilo.

Alisema moja ya matukio makubwa yatakayofanyika ni uzinduzi wa Mfumo Jumuishi wa Maktaba Mtandao ya Taifa (Integrated National Digital Library System), pamoja na programu tumishi itakayowawezesha wananchi kupata huduma za maktaba kupitia simu za mkononi. Hatua hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa machapisho na taarifa kwa kutumia teknolojia, sambamba na mwelekeo wa taifa wa kuimarisha matumizi ya kidijitali.

Dkt. Ruzegea alifafanua kuwa mfumo huo hautamaanisha kila kitabu kitapatikana chote mtandaoni, akisema machapisho yanayolindwa na hakimiliki yatahitaji utaratibu maalumu wa makubaliano na wenye haki hizo. Aidha, kongamano hilo litatambulisha maboresho ya sheria ya huduma za maktaba na kanuni zake, zitakazowapa wadau nafasi ya kutoa maoni kuhusu utekelezaji wa huduma hizo katika mazingira ya kidijitali.

Alisema maktaba za ana kwa ana, zikiwemo za mikoa, wilaya na jamii, zitaendelea kutoa huduma kwa wananchi wasio na intaneti, huku kongamano likijadili namna ya kuziimarisha kwa kuzipatia vitabu, wataalamu na mazingira bora ya kujifunzia. Aliongeza kuwa taasisi zitaunganishwa kwenye mfumo wa kidijitali kwa awamu kulingana na utayari wake.

Kongamano hilo pia litaambatana na Tamasha la Vitabu na Usomaji, maonyesho ya machapisho na mijadala kuhusu maendeleo ya maktaba za jamii. Vilevile, litaadhimisha miaka 37 ya chuo cha mafunzo ya ukutubi kinachohusishwa na TLSB, pamoja na kuanzisha jukwaa la Partnership Marketplace litakalowakutanisha wadau na washirika kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maktaba.

Dkt. Ruzegea alisema kongamano hilo litafuatia mkutano wa siku moja wa wakutubi wakuu kutoka taasisi za serikali na binafsi, utakaofanyika Oktoba 19 kujadili uendeshaji wa huduma za maktaba. Alisema baada ya kongamano, maazimio yatakayofikiwa yatawekewa vipimo na kufuatiliwa ili kuhakikisha yanatekelezwa. Kongamano hilo ni la nne baada ya yaliyofanyika mwaka 2021, 2022 na 2023, na ushiriki wake ni bure kwa wananchi na wadau wote.