Dodoma, Oktoba 17, 2026. Baraza la Sita la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) limehitimishwa mkoani Dodoma baada ya kudumu kwa siku mbili, likiwa na lengo la kujadili masuala ya wafanyakazi na kuimarisha utendaji wa kazi. Katika baraza hilo, wafanyakazi wamepatiwa mafunzo ya afya ya akili yaliyotolewa na Daktari Bingwa wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dkt. Garvin Kweka, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa afya ya akili katika mazingira ya kazi na maisha ya kila siku.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea wafanyakazi uelewa kuhusu namna ya kutambua na kukabiliana na msongo wa mawazo, kutunza afya ya akili na kuimarisha ustawi wao. Elimu hiyo inatarajiwa kuwasaidia wafanyakazi kukabiliana na changamoto za kikazi, kuboresha mahusiano kazini na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya kuhudumia wakulima, wafanyabiashara na wadau wengine wa sekta ya kilimo.
Akifunga baraza hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph C. Ndunguru, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia ustawi wa wafanyakazi sambamba na kuboresha utendaji wa Mamlaka. Baraza hilo limekuwa fursa ya kujadili masuala ya wafanyakazi na mikakati ya kuboresha mazingira ya kazi, hatua inayolenga kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
