📍DODOMA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini,Msafiri Mbibo, amesisitiza umuhimu wa wafanyakazi wa Wizara ya Madini, taasisi zake na sekta ya madini kufanya mazoezi mara kwa mara ili kulinda afya na kuongeza tija katika utendaji wa kazi.

Akizungumza Oktoba 17, 2026 katika Viwanja vya Shule ya Sekondari John Merlin, Mipango Dodoma, wakati wa Madini Bonanza 2026 lililoandaliwa na Taasisi ya TEITI kwa kaulimbiu “Michezo ni Furaha na Afya,” Mbibo amesema sekta ya madini ni muhimu katika ujenzi wa uchumi wa taifa, utoaji wa ajira na kuboresha maisha ya Watanzania.

Amesema kutokana na umuhimu huo, ni muhimu watumishi katika sekta hiyo kuwa na afya njema ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kupunguza matumizi ya huduma za hospitali na gharama za matibabu.

Mbibo amesema kulinda afya ni bora kuliko kusubiri tiba, akisisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari na shinikizo la damu.

Aidha, amebainisha kuwa afya njema ya wafanyakazi husaidia kuongeza tija kazini, ubunifu, kujituma na weledi, huku watumishi wakiwa katika hali nzuri ya kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Amesema Serikali inaendelea kuweka programu mbalimbali za kuimarisha afya, ikiwemo bima ya afya, lakini amesisitiza kuwa watumishi wanapaswa pia kuchukua hatua binafsi za kulinda afya zao.

Mbibo amesisitiza kuwa programu za mazoezi hazipaswi kuwa tukio la siku moja kwa ajili ya kupiga picha, bali ziwe endelevu ili kusaidia kufikia matokeo ya kweli katika kulinda afya za watumishi.

Kwa upande wake, Afisa Rasilimali Watu wa Tume ya Madini, Omari Sebabili, amesema bonanza hilo lina tija katika kuboresha afya za watumishi, kuwaweka katika utimamu wa mwili na kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.