Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo

WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameiagiza Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Mkoa wa Pwani na Wilaya ya Bagamoyo, kuharakisha tathmini na ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopisha eneo la mradi wa uwekezaji Zinga,Bagamoyo.

Eneo hilo lina ukubwa wa hekta 887 ambao baadhi yao wamesubiri haki zao kwa takriban miaka 16.

Aidha, Mwigulu ameitaka Wizara ya Ardhi kuhakikisha kuwa baada ya kukamilika kwa zoezi la uthamini, inapima mipaka ya maeneo husika na kutoa hati za umiliki ili kuondoa migogoro na kuweka mazingira bora kwa shughuli za uwekezaji.

Akizungumza Oktoba 16, 2026, katika Kongani ya HWTZ SEZ iliyopo kwenye eneo maalum la uwekezaji la kiuchumi la TISEZA, Bagamoyo, Mwigulu alisema Serikali imeweka utaratibu maalumu wa kushughulikia changamoto za wananchi waliopisha maeneo kwa ajili ya miradi ya maendeleo lakini hawajalipwa fidia kwa muda mrefu.

Alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kulipwa haki zao ili kumaliza malalamiko na migogoro ya ardhi, huku shughuli za uwekezaji zikiendelea katika mazingira ya amani na ushirikiano.

“Mkoa wa Pwani umetutoa kimasomaso, muendelee na kasi hiyohiyo katika kuinua sekta ya uwekezaji na viwanda,” anasema Mwigulu.

“Mvua ya El Niño isiwe kigezo na sababu, kila shughuli inasimama kisa mvua, Muendelee na kazi, siyo tunasubiria kama harusi,” alisema Mwigulu.

Katika hatua nyingine, Mwigulu anasisitiza kukamilishwa kwa haraka kwa eneo maalumu la hekari 50 lililotengwa na TISEZA kwa ajili ya vijana, akieleza umuhimu wa kuwawezesha kunufaika na fursa za uwekezaji na viwanda.

Waziri Mkuu amefafanua, uwekezaji katika Kongani ya Viwanda ya HWTZ ni sehemu ya jitihada za Serikali za kukuza uchumi wa viwanda na kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja.

MKUU WA MKOA WA PWANI

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema mkoa huo unaendelea kupokea wawekezaji kutokana na juhudi za kuboresha mazingira ya uwekezaji, sambamba na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Nyongo amesema Mkoa wa Pwani una jumla ya viwanda 1,768, vikiwemo viwanda vikubwa 503, vya kati 248 na vidogo 1,017, huku ukiwa na kongani 35 za viwanda, ikiwemo HWTZ SEZ.

Kuhusu upatikanaji wa nishati ya umeme, amesema vijiji vyote 409 vya mkoa huo vimefikiwa na huduma hiyo, huku kazi ya kusambaza umeme katika vitongoji ikiendelea ambapo mkoa unatarajia kufikia asilimia 95 ya vitongoji vilivyounganishwa na umeme ifikapo Desemba 2026.

Kuhusu changamoto za ardhi, Nyongo amesema Serikali mkoani humo inaendelea kuchukua hatua dhidi ya matapeli na wavamizi wa maeneo ya ardhi, huku ikiendelea kushughulikia migogoro inayohusisha wakulima na wafugaji.

MBUNGE BAGAMOYO

Akizungumzia changamoto za wananchi, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Subira Mgalu, ameiomba Serikali kusimamia kwa karibu ulipaji wa fidia kwa wananchi ambao wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu, akieleza kuwa waliahidiwa pia kupatiwa maeneo baada ya kulipwa fidia.

Mgalu amewasilisha pia changamoto nyingine za jimbo hilo, zikiwemo migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji pamoja na ombi la kuboresha kwa kiwango cha lami barabara ya Makofia–Mlandizi–Mzenga na Tamco-Mapinga.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa TISEZA, Anna Lyimo, alisema kutengwa kwa maeneo maalumu ya uwekezaji kutafungua fursa kubwa za kiuchumi na kuongeza ajira, hususan kwa vijana.

Lyimo alisema katika eneo hilo, viwanda 150 vinatarajiwa kuendelezwa, ambapo hadi sasa viwanda 25 vimefikia hatua mbalimbali za ujenzi ikiwemo HWTZ SEZ, 10 vimekamilika ambapo uwekezaji utakaochochea shughuli za kiuchumi na kuongeza fursa za ajira.

Akifafanua kuhusu malipo ya fidia katika eneo la mradi lenye ukubwa wa hekta 887, huku wananchi 1,154 wakiwa wamelipwa ,wananchi 4,005 ambao mali zao zilifanyiwa tathmini takriban miaka 16 iliyopita bado hawajalipwa, huku wengine 1,130 hivyo jumla ya wananchi 5,135 ambao bado wanahitaji kushughulikiwa fidia.

Naye Mkurugenzi wa HWTZ SEZ, Sophia Su, amesema kongani hiyo inatarajia kujenga viwanda 150, ambapo viwanda saba vitajengwa na kampuni hiyo.

Amesema hadi sasa shughuli za kiwanda hicho zimezalisha ajira 170 katika maeneo mbalimbali, huku idadi hiyo ikitarajiwa kufikia ajira 400 ifikapo Desemba 2026