NA SOPHIA KINGIMALI, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limeongeza mapato yake kutoka Sh bilioni 1.3 hadi takribani Sh bilioni 147.8 katika mwaka wa fedha 2025/26, hatua inayodhihirisha mafanikio ya mageuzi yaliyofanyika katika shirika hilo na kupunguza utegemezi wa fedha kutoka serikalini.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mtendaji STAMICO,Dkt CPA Venance Mwasse amesema ongezeko hilo limetokana na mabadiliko ya kiutendaji, uwekezaji katika miradi ya madini, ubia na kampuni nyingine pamoja na kuimarisha usimamizi wa shughuli za shirika.

Amesema awali shirika lilikuwa likitegemea serikali kwa takribani asilimia 89 ya mahitaji yake, lakini baada ya mageuzi limeimarisha uwezo wake wa kujiendesha, kugharamia mishahara ya watumishi na kuchangia mapato ya serikali.

Ameeleza kuwa STAMICO, iliyoanzishwa mwaka 1972 na inayomilikiwa kwa asilimia 100 na serikali, ina jukumu la kushiriki katika mnyororo mzima wa thamani wa madini kwa niaba ya Watanzania, kuanzia utafiti, uchimbaji, uchenjuaji, uongezaji thamani hadi biashara ya madini.

Amesema kuanzishwa kwa shirika hilo kulilenga kuhakikisha nchi haishiriki katika ukusanyaji wa kodi pekee kutoka kwa wawekezaji, bali pia inapata manufaa ya moja kwa moja kupitia uwekezaji na uzalishaji wa rasilimali zake huku akiongeza kuwa ushiriki huo unaimarisha uwezo wa serikali kuelewa changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya madini.

Aidha CPA Mwasse amesema Shirika limefanya mageuzi makubwa kuanzia mwaka 2020 na yamekuwa msingi wa mafanikio ya sasa, yakilenga kubadili fikra, mifumo ya uendeshaji na kuongeza uwekezaji katika miradi yenye uwezo wa kuingiza mapato na kutengeneza ajira kwa Watanzania.

Pia,ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuongezeka kwa idadi ya watumishi kutoka takribani 111 hadi karibu 800, huku shirika likipanua shughuli zake za utafiti, uchimbaji na utoaji wa huduma za kitaalamu kwa kampuni zinazofanya shughuli za madini nchini.

Katika hatua nyingine, amesema STAMICO imeendelea kuimarisha miradi ya kimkakati na kuingia mikataba minne ya ubia katika miradi inayohusisha madini muhimu, yakiwamo ya kimkakati yanayohitajika katika uchumi wa dunia amesema miradi hiyo inalenga kuhakikisha nchi inanufaika na fursa zinazotokana na ongezeko la mahitaji ya madini hayo.

Ametaja mradi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Songwe, kuwa miongoni mwa miradi ambayo shirika limeendelea kuifanyia maboresho baada ya kukumbwa na changamoto za uzalishaji akisema maboresho ya mitambo na miundombinu ni sehemu ya juhudi za kuongeza tija na kurejesha uhai wa miradi hiyo.

Kuhusu kuwawezesha wachimbaji wadogo, amesema STAMICO imeongeza uwekezaji katika vifaa na huduma za kitaalamu, ikiwamo kuongeza mitambo ya uchorongaji kutoka mitatu hadi 18 na kuweka mitambo 17 kwa ajili ya kusaidia shughuli za wachimbaji wadogo. Pia shirika limeendelea kutoa mafunzo na kuwasaidia wachimbaji kuboresha mbinu za uzalishaji.

Amesema shirika linaendelea kusaidia makundi mbalimbali ya wachimbaji wadogo, wakiwamo wanawake na vijana, kupitia mafunzo, ushauri wa kitaalamu na vifaa. Ametoa mfano wa kundi la wanawake wachimbaji lililosaidiwa kwa kupewa pampu 10 kati ya 18 walizoomba ili kukabiliana na changamoto ya maji katika maeneo yao ya uchimbaji.

Akijibu maswali ya wahariri kuhusu masoko ya madini, alisema STAMICO ina mtandao wa masoko 44 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini takribani 120, ambavyo vimesaidia kuwarahisishia wachimbaji na wafanyabiashara kupata maeneo rasmi ya kuuza madini ambapo mfumo huo pia unasaidia kupunguza mianya ya utoroshaji wa madini na kuongeza mapato yanayokusanywa nchini.

Kuhusu upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo, amesema shirika linaendelea kushughulikia changamoto za upatikanaji wa mitaji na kwamba mchakato wa kuanzisha Benki ya Wachimbaji Tanzania umeanza kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo ambapo benki hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa fedha na kuwezesha Watanzania kushiriki zaidi katika shughuli za uchimbaji.

Aidha, amesema STAMICO inaendelea kushiriki katika miradi ya ubia ambapo shirika huchangia leseni na utafiti wa awali, huku washirika wakileta mtaji na teknolojia, kisha faida na manufaa ya mradi kugawanywa kwa mujibu wa makubaliano amesisitiza kuwa shirika ni mwekezaji katika sekta ya madini na si mdhibiti, jukumu ambalo linatekelezwa na taasisi husika za serikali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile, amesema mafanikio ya STAMICO yanaonyesha kuwa taasisi za umma zinaweza kuimarika na kuongeza tija zinapotekeleza mageuzi na kusimamia rasilimali kwa ufanisi. Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa shirika kuimarisha utafiti na ukusanyaji wa takwimu za kisasa ili mafanikio yake yaweze kupimwa kwa taarifa sahihi na za wakati, huku akiwataka wahariri kuendelea kufuatilia miradi ya madini na kuelimisha umma kuhusu mchango wake katika uchumi wa taifa.