Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamsaka mtu anayetajwa kwa jina la Peter Kiariro, mkazi wa Maore, Wilaya ya Same, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Bernard Kiluwa, mwenye umri wa miaka 26, mkazi wa Kijiji cha Mheza, Kata ya Maore, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.
Tukio hilo limetokea Oktoba 12, 2026, majira ya usiku, katika Kitongoji cha Kalemane, Kijiji cha Mheza, Kata ya Maore, Tarafa ya Ndungu, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.
Uchunguzi wa awali umebainisha chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi baada ya marehemu kucheza muziki kwa muda mrefu na mke wa mtuhumiwa wakati wa sherehe ya ubarikio iliyokuwa ikifanyika nyumbani kwa Shabani Rajab.
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alimwomba marehemu waende pembeni kwa ajili ya mazungumzo, lakini baadaye alimshambulia kwa kutumia kitu chenye ncha kali kinachodhaniwa kuwa kisu, na kumjeruhi tumboni na kifuani kabla ya kutoroka eneo la tukio.
Kutokana na hali yake kuwa mbaya, alipelekwa Kituo cha Afya Ndungu kwa matibabu zaidi ambako alifariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu.
Juhudi za kumtafuta na kumkamata mtuhumiwa ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe.
Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro linatoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa mtuhumiwa kutoa taarifa katika kituo cha Polisi.
