Na: Farida Mangube
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Cardiff nchini Uingereza umebainisha kuwa matumizi ya visima binafsi vya maji chini ya ardhi yamekuwa sehemu muhimu ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji katika Jiji la Dodoma, huku ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi likiendelea kuongeza mahitaji ya huduma hiyo.
Matokeo ya utafiti huo, yaliyowasilishwa Oktoba 15, 2026, katika warsha ya kuwasilisha na kuhakiki matokeo ya utafiti mradi wa “Water Resilient Cities” iliyofanyika jijini Dodoma, yanaonesha kuwa zaidi ya asilimia 10 ya kaya zilizoshiriki katika utafiti zimeripoti kumiliki visima binafsi, huku idadi ya wananchi wanaotumia vyanzo hivyo ikiongezeka ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita.
Akiwasilisha matokeo hayo, Kiongozi wa Mradi kutoka Chuo Kikuu cha Cardiff nchini Uingereza Dkt. Adrian Healy amesema utafiti uliohusisha kaya 500 Januari 2024, pamoja na mahojiano ya kina katika kaya 54 Oktoba 2023, umebainisha kuwa kutopatikana kwa maji ya mabomba kwa uhakika ni sababu kuu inayowasukuma baadhi ya wananchi kuwekeza katika uchimbaji wa visima binafsi ili kukidhi mahitaji ya familia zao na kupunguza gharama za kununua maji.
Amesema matokeo yanaonesha kuwa asilimia 67 ya kaya zilizoulizwa kuhusu hatua zilizochukua kukabiliana na changamoto za maji ziliripoti kununua maji yanayosafirishwa kwa magari au mikokoteni, asilimia 63 kupunguza matumizi ya maji, asilimia 51 kuhifadhi maji kwenye matanki na asilimia 41 kushirikiana na majirani kupata huduma hiyo.
Aidha, asilimia 22 ziliripoti kuwekeza katika vyanzo vyao binafsi vya maji, ikiwemo visima.
Dkt. Healy ameeleza kuwa pamoja na visima binafsi kusaidia kupunguza gharama na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa maji, vimekuwa pia na mchango katika shughuli za kiuchumi na kijamii, hususan katika maeneo ambayo mtandao wa maji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) haujafika au haukidhi mahitaji ya wananchi ikififikia tu asilimia 55 ya mahitaji.
Hata hivyo, amesema matumizi hayo yanahitaji usimamizi madhubuti kutokana na uwezekano wa kuchotwa kwa maji mengi kuliko uwezo wa vyanzo kujazwa upya, pamoja na changamoto za ubora wa maji.
Amebainisha kuwa wananchi wengi wanaotumia maji ya visima hutathmini ubora wake kwa kuangalia ladha na mwonekano badala ya kufanya vipimo vya kitaalamu, jambo linaloweza kuhatarisha afya endapo maji yatakuwa na uchafuzi usioonekana.
Akizungumzia ongezeko la mahitaji ya maji jijini Dodoma, Dkt. Healy amesema takwimu zilizowasilishwa katika utafiti zinaonesha mahitaji ya maji yakifikia mita za ujazo 159,000 kwa siku mwaka 2026, huku makadirio yakionesha kuwa yanaweza kufikia mita za ujazo 250,000 kwa siku ifikapo mwaka 2035 na mita za ujazo 400,000 kwa siku mwaka 2050.
Hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuimarisha vyanzo vilivyopo na kutafuta mifumo mbadala ya kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji.
Aidha, amependekeza kuangaliwa kwa uwezekano wa kutumia mfumo mchanganyiko wa usambazaji wa maji unaounganisha mtandao rasmi wa mabomba, visima binafsi na teknolojia za kurejeleza maji yaliyotumika kwa shughuli zisizohitaji maji ya kunywa.
Amesema uzoefu wa miji ya Cape Town nchini Afrika Kusini na Windhoek nchini Namibia unaonesha namna matumizi ya maji chini ya ardhi na uhifadhi wake yanavyoweza kusaidia miji kukabiliana na ukame na changamoto za upatikanaji wa maji.
Kwa upande wa Serikali, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji katika Wizara ya Maji, Mhandisi Robert Sunday, amesisitiza umuhimu wa tafiti za kisayansi katika kuimarisha usalama wa maji nchini, akieleza kuwa matokeo ya tafiti hizo yanapaswa kutumika katika kuboresha sera, mipango na mikakati ya usimamizi wa rasilimali za maji, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema maendeleo endelevu ya miji yanategemea upatikanaji wa maji ya uhakika kwa matumizi ya kijamii na shughuli za kiuchumi, hivyo ni muhimu kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, vyuo vikuu na taasisi za utafiti ili kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatumika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Utafiti huo, ambao ni sehemu ya tafiti zinazofanyika katika miji minne ya Afrika ikiwemo Dodoma, Cape Town, Windhoek na Lagos nchini Nigeria, unatarajiwa kutoa maarifa yatakayosaidia kuboresha usimamizi wa maji chini ya ardhi na kuimarisha ustahimilivu wa miji dhidi ya changamoto za upungufu wa maji, huku ukichangia jitihada za Tanzania kufikia malengo ya dira ya maendeleo ya mwaka 2050

