Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (KCRI), Profesa Blandina Mmbaga akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano huo jijini Arusha .
………..
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha.Mkurugenzi idara ya afya ya uzazi mama na mtoto wizara ya afya Dkt.Ahmad Makuwani amesema kuwa, upatikanaji wa takwimu sahihi kupitia daftari la wagonjwa wa saratani ni hatua muhimu katika kuboresha mipango na huduma za matibabu ya ugonjwa huo nchini.
Amesema matumizi ya daftari hilo yanalenga kuondoa utegemezi wa takwimu za makadirio na badala yake kuweka mfumo unaotumia taarifa halisi kuhusu wagonjwa wa saratani, hali itakayosaidia kupanga mikakati madhubuti ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Ameyasema hayo leo.jijini Arusha kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara ya Afya wakati akizungumza kwenye mkutano wa Kwanza wa Pamoja wa Kisayansi wa Mitandao Mitatu ya Kimataifa ya Ufuatiliaji na Utafiti wa Saratani Jijini Arusha.
Aidha mkutano huo umewakutanisha wadau kutoka sehemu mbalimbali duniani na barani Afrika ukiwa ni fursa kwa Tanzania kujifunza uzoefu na mbinu bora zinazoweza kutumika kuboresha huduma za saratani, hususani saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti.
Dkt. Makuwani amesema takwimu hizo zitasaidia kubaini aina mbalimbali za saratani zinazowakabili wananchi, maeneo yenye wagonjwa wengi, makundi ya umri yanayoathirika pamoja na sababu zinazoweza kuchangia kuenea kwa magonjwa hayo, hivyo kuwezesha wataalamu kupanga hatua zinazofaa za kinga, uchunguzi na matibabu.
Ameongeza kuwa taarifa sahihi ni msingi wa kufanya maamuzi ya kisera na kupanga rasilimali zinazohitajika katika sekta ya afya, ikiwemo idadi ya watumishi wenye ujuzi na weledi, upatikanaji wa dawa pamoja na vifaa tiba kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
Dkt.Makuwani mesema uwepo wa takwimu zinazotegemewa utaisaidia Serikali kuelekeza rasilimali katika maeneo yenye uhitaji mkubwa na kuboresha utoaji wa huduma kulingana na mahitaji halisi ya wagonjwa, badala ya kutegemea makadirio ambayo yanaweza yasioneshe hali halisi ya ugonjwa huo.
Dk. Makuwani amezipongeza taasisi za KCMC na KCRI kwa kushirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi katika juhudi za kuimarisha ukusanyaji na matumizi ya takwimu za saratani, akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuongeza uelewa na kuimarisha mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo.
“Kuimarika kwa takwimu kutasaidia kupanga vizuri upanuzi wa huduma za saratani zinazotolewa katika vituo mbalimbali nchini, vikiwemo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, KCMC na Hospitali ya Rufaa ya Bugando, ili kuhakikisha huduma hizo zinapangwa kulingana na mahitaji ya wananchi.”amesema Dkt.Makuwani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (KCRI), Profesa Blandina Mmbaga, kilichopo chini ya Hospitali ya Rufaa ya KCMC, amesema kongamano hilo limewakutanisha wataalamu na wabobezi wa masuala ya saratani, hususan saratani ya shingo ya kizazi, matiti na aina mbalimbali za saratani.
Profesa Mmbaga amesema lengo kubwa la kongamano hilo ni kujadili namna bora ya kutunza na kutumia takwimu za saratani katika nchi mbalimbali, ili kusaidia katika kupanga mikakati ya kinga, uchunguzi na matibabu ya ugonjwa huo.
Amesema jumla ya nchi 25 kutoka bara la Ulaya zimeshiriki katika kongamano hilo, sambamba na takribani nchi 35 kutoka bara la Afrika, ambapo wataalamu hao wamekutana kujadili changamoto zinazowakabili katika udhibiti wa saratani.
“Kupitia kongamano hili wataalamu wanaangalia umuhimu wa kuwa na takwimu za wagonjwa Ili kubaini ukubwa wa tatizo la saratani, ikiwemo kubaini aina za saratani zinazoongoza, maeneo ambayo ugonjwa huo umeenea zaidi pamoja na makundi ya umri yanayoathirika, ili wagonjwa wanaogundulika waweze kupata matibabu mapema”amesema Profesa Mmbaga.
Ameongeza kuwa katika kufanikisha azma hiyo, wataalamu kutoka KCRI wamekuwa wakishirikiana pia na waganga wa jadi, kwa kuwa baadhi ya wagonjwa baada ya kugundulika wamekuwa wakikimbilia kwao.
Naye Mkurugenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya kaskazini KCMC ,Prof. Gileard Masenga amesema magonjwa yasiyoambukiza yanaendelea kuongoza miongoni mwa wagonjwa wanaofika hospitalini kupata huduma za afya, ambapo kati ya wagonjwa 10, takribani wanane hugundulika kuwa na magonjwa hayo, ikiwemo saratani, shinikizo la damu, kisukari na madhara yatokanayo na ajali.
Prof. Masenga, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya, hususan katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, akieleza kuwa Juni 20 mwaka huu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua huduma ya tiba ya mionzi kwa wagonjwa wa saratani. Amesema kwa sasa KCMC wanaendelea kutoa matibabu ya saratani kwa kutumia mionzi.

