Na Jeremia Mwakyoma na Gladys Lukindo
DODOMA – OKTOBA 15, 2026
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imewajengea uwezo wajumbe wake wote wa menejimenti kupitia mafunzo ya uongozi yanayolenga kuwafanya kuwa viongozi wenye uwajibikaji na mwelekeo wa mabadiliko chanya.
Akifungua mafunzo hayo na kutoa mada, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi amewataka Wakurugenzi na Wakuu wa Idara wa BMH kubadilika kutoka kuwa wasimamizi wa shughuli za kila siku na kuwa viongozi wenye uwezo wa kukabiliana na mabadiliko, kufikiri kimkakati, kubuni na kuleta ubunifu, pamoja na kuelekeza juhudi katika kufikia matokeo yaliyokusudiwa.
“BMH tunahitaji uongozi wa kimkakati na Unaokabiliana na mabadiliko, changamoto na mazingira yasiyotabilika kwa kuhamasisha na kuwahusisha watumishi wa BMH kwa pamoja na kila mmoja kutoa mchango wake katika kutatua changamoto zilizopo na kufikia malengo ya pamoja yaliyopangwa (Strategic and Adoptive Leadership)” alisisitiza Prof. Makubi.
Prof. Makubi aliwasisitiza viongozi hao wa BMH kutambua kuwa ni lazima walete matokeo yanayoonekana na yanayogusa watu, huku akiwataka kugeuza miundombinu mizuri iliyopo kuleta matokeo bora (Better Outcomes) kwa kila kila idara kuchangia kuleta imani kwa wagonjwa.
“Hii itatusaidia kwenda mbele kimakakati na siyo ule utaratibu wa kazi za kawaida kila siku, inabidi kufikilia miaka mingi mbeleni, kutatua changamoto zetu hata zile ngumu, lazima tufikirie katika Muktadha wa kidunia (global thinking), tujenge team work, mashirikiano na mahusiano ya ndani na nje kimataifa, kutafuta rasilimali, kushiriki kimataifa ikiwemo katika tafiti” alifafanua Prof Makubi.
Aliwataka wajumbe hao wa.menejimenti na watumishi wa BMH kutambua wananchi leo hii wana matamanio makubwa ya kupata huduma bora za Afya, kiwango cha juu cha customer care, mawasiliano ya karibu, muda mfupi wa kupata huduma, kupata dawa zote na vifaa tiba.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa idara ya udhibiti ubora BMH Dkt. Paul Kazungu amepongeza idara zilizopata ithibati za kimataifa na kusisitiza idara nyingine zilizobakia nazo zinafikia hatua ya kupata ithibati hizo.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya wanawake na upandikizaji mimba BMH Cuthbert Magomba ameshauri BMH kufanya tathimin ya watoa huduma za Afya, kuona huduma zinazotolewa na mapungufu yaliyopo ili BMH iweze kuja na ubunifu wa huduma za kisasa zaidi katika Dunia ya leo ambazo zinaweza zisitolewe na Hospitali nyingine.
Akitoa mchango wake, Mkuu wa idara ya wagonjwa wa nje (OPD) Dkt. Mugisha Nkoronko amewataka wajumbe wengine kutambua kuwa viongozi bora wanatengenezwa, mafunzo hayo waliyopatiwa ni mkakati wa kutengeneneza viongozi watakaoleta mageuzi ya BMH na sekta ya Afya kwa ujumla.

