Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeimarisha ushirikiano na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwawezesha wabunge wanaoliwakilisha taifa katika mabunge na majukwaa ya kikanda na kimataifa kutetea ajenda na maslahi ya nchi. 

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma Oktoba 15, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Bw. Charles Kadonya wakati anawasilisha taarifa ya Wizara hiyo kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) chini ya mwenyekiti wake, Mhe. Najma Murtaza Giga.

Bw. Kadonya amesema Wizara yake imeandaa mwongozo maalumu uliokamilishwa Aprili 2025 kwa ushirikiano na Ofisi ya Bunge, kwa lengo la kuboresha uratibu, upatikanaji wa taarifa kwa wakati na maandalizi ya misimamo ya Tanzania katika mijadala ya kimataifa. Mwongozo huo ulitokana na maelekezo ya Kamati husika ya Bunge ya Agosti 2024, kufuatia changamoto za wawakilishi kukosa ratiba na taarifa za shughuli za majukwaa wanayoshiriki.

Tanzania ni mwanachama wa majukwaa saba ya kibunge ambayo ni Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Jukwaa la Kibunge la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF), Bunge la Afrika (PAP), Jukwaa la Kibunge la Maziwa Makuu (FP-ICGLR), Umoja wa Mabunge wa Nchi za Afrika, Karibe, Pasifiki na Jumuiya ya Ulaya (OACPS-EU), Chama cha Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Madola (CPA) na Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

Kupitia majukwaa hayo, wawakilishi wa Tanzania wana wajibu wa kufuatilia mijadala ya sera, miswada na maazimio, kupata misimamo rasmi ya Serikali na kuitetea, pamoja na kubaini athari zinazoweza kuikabili nchi. 

Jitihada hizo zinaendana na Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001, Toleo la mwaka 2024, inayosisitiza ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika kulinda na kuendeleza maslahi ya Tanzania kisiasa, kiuchumi, kiulinzi na kijamii. 

Wajumbe wa Kamati ya NUU, licha ya kupongeza juhudi za Wizara za kuandaa Mwongozo Maalum, walifurahishwa pia namna Wizara hiyo ilivyoratibu kwa mafanikio makubwa Mkutano wa 153 wa IPU uliofanyika Arusha Oktoba 5 – 9, 2026. Walisema mafanikio ya mkutano huo ni kielelezo cha wazi cha kuimarika kwa diplomasia ya Tanzania chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.