– NDEJEMBI AIPONGEZA

Makamu wa Rais na Waziri wa Vijana wapongeza mafanikio ya mikataba 3,466 kwa vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu

Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imepongezwa kwa kuwezesha makundi maalum ya Watanzania kushiriki katika fursa za ununuzi wa umma, baada ya makundi 33,524 ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu kusajiliwa na kunufaika na mikataba 3,466 yenye thamani ya Sh bilioni 74.32 katika kipindi cha kuanzia Julai 1, 2023 hadi Oktoba 13, 2026.

Takwimu hizo ziliwasilishwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, katika ripoti yake wakati wa kilele cha mbio hizo kilichofanyika Oktoba 14, 2026 katika Uwanja wa CCM Nelson Mandela mjini Sumbawanga Mkoani Rukwa

Katika hotuba ya kufunga mbio hizo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, aliipongeza PPRA kwa kuimarisha mifumo inayowawezesha wananchi kupata fursa za zabuni za Serikali.

“Ninaisifu sana PPRA kwa hatua kubwa na za mfano walizochukua katika kuwezesha fursa za ununuzi wa umma kwa wananchi wetu.

Kuona kwamba zaidi ya makundi 33,500 ya wananchi yamesajiliwa na kupata fursa za mikataba ya zabuni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 74.32 ni ushahidi thabiti kuwa Serikali inafanya kazi kwa ajili ya Watanzania wote,” alisema Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi.

Takwimu zilizowasilishwa katika ripoti hiyo zinaonesha kuwa vijana wanaongoza kwa idadi ya makundi yaliyosajiliwa, wakiwa 16,582, wakifuatiwa na wanawake 15,412, wazee 789 na watu wenye ulemavu 741.

Katika upande wa mikataba, vijana wamepata mikataba 2,066 yenye thamani ya Sh bilioni 40.56, huku wanawake wakipata mikataba 1,264 yenye thamani ya Sh bilioni 29.76.

Wazee wamepata mikataba 93 yenye thamani ya Sh bilioni 3.36, huku watu wenye ulemavu wakipata mikataba 43 yenye thamani ya Sh milioni 635.7.

 Kwa jumla, mikataba 3,466 yenye thamani ya Sh bilioni 74.32 imeripotiwa kutolewa kwa makundi hayo katika kipindi husika.

Akitoa pongezi zake, Waziri mwenye dhamana ya vijana, Mhe. Joel Nanauka, alisema juhudi za PPRA zimechangia kufungua fursa za kiuchumi kwa vijana kupitia zabuni na kandarasi za umma.

“Vijana ndio nguvu kazi kuu ya taifa hili. Ripoti za ununuzi wa umma zilizosimamiwa na PPRA zinaonyesha wazi jinsi milango ya fursa ilivyofunguka.

Zaidi ya mikataba 2,000 yenye thamani inayozidi Shilingi Bilioni 40 imekwenda mikononi mwa vijana wetu. Hili ni fanikio kubwa mno linalostahili pongezi za dhati,” alisema Mhe. Nanauka.

PPRA imeendelea kuhamasisha vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu nchini kote kujisajili katika mifumo rasmi ya ununuzi wa umma na kufuatilia fursa za zabuni zinazotangazwa na taasisi nunuzi.

Mamlaka inasisitiza umuhimu wa uwazi, uwajibikaji na ushiriki mpana wa wananchi katika michakato ya ununuzi wa umma kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazotumika.