Greda likiendelea na ya kuchonga Barabara ya Lukalasi-Machimba katika Halmashauri ya wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma.
Na Mwandishi wetu,Mbinga
HALMASHAURI ya wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma,imeanza kuzifungua na kufanya ukarabati barabara za kimkakati zinazounganisha maeneo ya uzalishaji ili kuwezesha wananchi kufika kusikofikika,kurahisisha usafiri na usafiri kwa lengo la kuchochea kasi ya uchumi wa wananchi na Halmashauri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Joseph Kashushura,ametaja barabara zilizoanza kufunguliwa ni Amanimakolo-Kiwombi,Mkulumusi-Machimbo-Lukalasi yenye urefu wa kilometa 18 ambayo imefunguliwa ili wananchi hususani wakulima wa maeneo hayo waweze kupitisha mazao hasa mahindi kutoka mashambani na kupeleka kwenye masoko.
“Barabara hizi zilikuwa na shida sana,kwahiyo tumeamua kuzifungua kwa kuzichonga na kutengeneza kwa kiwango cha changarawe ili ziweze kupitika kwa lengo la kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao yanayolimwa katika maeneo hayo”alisema Kashushura.
Alitaja barabara nyingine zilizoko kwenye mpango huo ni Matiri-Lukiti Linda inayopita kwenye maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa zao la kahawa ambapo alieleza,barabara hiyo itachochea kukua kwa uchumi wa wananchi na Serikali kwa ujumla kupitia zao la kahawa.
Alisema,mpango huo ni endelevu na katika awamu ya kwanza unahusisha barabara zenye urefu wa kilometa 49.5 kwa kuwa barabara ni uchumi kwani bila kuwa na barabara zinazopita kirahisi itakuwa tatizo kwa wananchi wa Halmashauri ya wilaya Mbinga kuendesha na kufanya shughuli za maendeleo.
“Halmashauri tupo kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanatekeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi kwenye mazingira rafiki badala ya kuwa kikwazo,tunawaomba wananchi waendelee kutuunga mkono kwenye utekelezaji wa mpango huo maalum”alisema Kashushura.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa kata ya Kigonsera,wameeleza kuwa ufunguzi na ujenzi wa barabara hizo utafungua fursa mpya za kilimo na biashara katika maeneo yao ambayo kwa miaka mingi yalikuwa yanakabiliwa na changamoto ya miundombinu mibovu ya barabara.
Mkazi wa kijiji cha Kigonsera Gelod Komba,ameipongeza Halmashauri ya wilaya Mbinga kuanza kuboresha miundombinu ya barabara zake zinazounganisha maeneo mbalimbali ya uzalishaji.
Alisema,kwa muda mrefu barabara ya Mkulumusi-Lukalasi-Machimbo ilikuwa kwenye hali mbaya hivyo kusababisha wananchi hususani wakulima kutonufaika na shughuli wanazofanya kwani walilazimika kuuza mazao yakiwa shambani kwa bei ndogo baada ya kushindwa kupeleka kwenda kwenye masoko ya uhakika.
Ameiomba Halmashauri ya wilaya na Wakala wa barabara za mijini na vijijini(TARURA),wenye dhamana ya barabara kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika ili kuleta tija katika ujenzi wa barabara hizo.
Ameongeza kuwa,uboreshaji wa miundombinu hiyo umeanza kuleta matokeo chanya kwani wananchi wengi sasa wanaendelea kuwekeza katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo.
Christian Kapinga mkazi wa Mkulumusi alisema,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Halmashauri ya wilaya Mbinga kwenye utekelezaji wa uboreshaji wa barabara ambazo zina mchango mkubwa kiuchumi.
Alisema,awali walikuwa wanapitia changamoto nyingi wanapotaka kwenda makao makuu ya kata Kigonsera kwa ajili ya kupata huduma muhimu au Hospitali ya Halmashauri ya wilaya iliyopo eneo la hifadhi kupata matibabu kutokana na ubovu wa barabara.
Alisema,walikuwa wanapita kwa shida kutokana na barabara hiyo kuwa na mchanga mwingi wakati wa kiangazi na wakati wa masika hujaa maji hivyo kusababisha hata mama wajawazito kujifungulia njiani kabla ya kufika kituo cha afya Kigonsera.
Shanel Ndunguru mfanyabiashara wa mkaa,ameshauri barabara hiyo na nyingine zinazoendelea kufunguliwa kuwekwa kokoto ili wakati wa masika ziweze kupitika kirahisi na kutoa fursa kwa wananchi na wafanyabiasha waendelee na shughuli za kiuchumi.
