● Waziri Mavunde aeleza mkakati wa kudhibiti utoroshaji na kukuza biashara ya Tanzanite

● Serikali kuongeza utafiti wa kina eneo la Mirerani kuwasaidia wachimbaji

● Kamati ya Bunge yaitaka Serikali kuongeza nguvu kuitangaza Tanzanite kimataifa

 

● Wizara yapongezwa kwa kuvuka lengo la makusanyo ya maduhuli Robo ya Kwanza (2026/2027)

 

Dodoma

Wizara ya Madini imewasilisha Bungeni mkakati kabambe unaolenga kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa uchimbaji, udhibiti, uongezaji thamani, na biashara ya madini ya Tanzanite nchini.

Akiwasilisha mkakati huo leo Oktoba 13, 2026, mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema kuwa mwenendo wa soko la Tanzanite duniani kwa sasa unakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo serikali inaendelea kuzifanyia kazi.

 Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni uwepo wa wafanyabiashara wa madini wasiofuata taratibu,kupungua kwa uzalishaji,utoroshaji wa madini hayo na ushindani mkubwa kutoka kwa vito mbadala vinavyotengenezwa viwandani (synthetic gemstones).

Mhe. Mavunde ameeleza kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali inafanya maboresho makubwa kwenye mfumo wa biashara wa ndani na wa kimataifa.

Katika mkakati huo, Serikali imejipanga kukamilisha ujenzi wa jengo maalum la biashara(Tanzanite Exchange Centre),kuweka mfumo rasmi wa minada ili kuhakikisha Tanzanite yote inaongezewa thamani nchini badala ya kusafirishwa ikiwa ghafi na serikali kufanya utafiti wa kina wa madini nje ya ukuta wa mirerani.

“Lengo letu ni kuwasaidia wachimbaji na wafanyabiashara wa vito wazawa kuuza madini yao kwa bei shindani inayoendana na soko la dunia. Tutaifikia bei hiyo kupitia mifumo thabiti ya siri na ya wazi ya uthaminishaji wa madini,” amesema Mhe. Mavunde.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amebainisha kuwa, Serikali itafanya utafiti wa kina katika eneo la Mirerani ili kugundua maeneo mapya yenye viashiria vya madini hayo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Subira Mgalu, ameishauri Serikali kuongeza nguvu na mikakati ya makusudi katika kuitangaza Tanzanite kwenye masoko makubwa ya kimataifa (Global Rebranding).

Mhe. Mgalu amesisitiza kuwa, kwa kuwa Tanzania ndiyo nchi pekee duniani inayozalisha Tanzanite, jina la nchi linapaswa kuonekana kwa uwazi kwenye mnyororo mzima wa thamani wa vito hivyo duniani ili nchi ipate tija inayostahili kiuchumi.

Pamoja na mambo mengine, Mhe. Mgalu ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kwa Robo ya Kwanza ya Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Katika Mwaka wa Fedha wa 2026/2027, Wizara ya Madini imepangiwa na inalenga kukusanya jumla ya Shilingi Trilioni 1.406, ambapo mwenendo wa robo ya kwanza unaonyesha mwelekeo mzuri wa kufikia na kuvuka lengo hilo.