Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mpanda mkoani Katavi, wakati akielekea Sumbawanga mkoani Rukwa kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2026 na Kumbukizi ya Miaka 27 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tarehe 13 Oktoba 2026

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi akicheza ngoma ya kabila la wafipa, wakati akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mpanda mkoani Katavi, akielekea Sumbawanga mkoani Rukwa kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2026 na Kumbukizi ya Miaka 27 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tarehe 13 Oktoba 2026.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwasalimia wananchi wa Mpanda, mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mpanda mkoani Katavi, akielekea Sumbawanga mkoani Rukwa kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2026 na Kumbukizi ya Miaka 27 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tarehe 13 Oktoba 2026.

……………

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi,ameagiza kuharakishwa kwa miradi ya barabara, maji na umeme mkoani Katavi, huku akiwataka wakandarasi wanaosuasua kuongeza kasi ya utekelezaji ili wananchi waanze kunufaika na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali.

Maagizo hayo ametoa alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Mpanda, akiwa njiani kuelekea Sumbawanga mkoani Rukwa kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, ambapo alipata fursa ya kuwasalimia wananchi waliojitokeza kumpokea.

Akizungumzia changamoto ya umeme, Makamu wa Rais ameitaka TANESCO kuhakikisha kufikia Desemba 01 2026, Mpanda inapelekewa Transfoma itakayoongeza megawati 50 zaidi za umeme ili kukidhi mahitaji yanayozidi kuongezeka katika Manispaa ya Mpanda na maeneo mengine ya mkoa huo.

Makamu wa Rais amesisitiza kuhakikisha ahadi ya kukamilisha maboresho hayo inatekelezwa, sambamba na kuweka nguzo za zege.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameonesha kutoridhishwa na kusuasua kwa ujenzi wa barabara za lami zenye thamani ya shilingi bilioni 29, akitaka kujua sababu za kuchelewa kwa kazi licha ya wakandarasi kuwa katika maeneo ya miradi.

Ameagiza mitambo kuingizwa kazini mara moja, huku akitaka hatua za haraka zichukuliwe katika barabara ya kuelekea Kigoma, hususani eneo la Mtonyamasi ambako ujenzi wa daraja na sehemu nyingine za barabara haujakamilika, hususani kwenye Kipindi hiki ambacho kumekuwa na tahadhari kubwa ya mvua za El-nino.

Pia ameelekeza kuharakishwa kwa ujenzi wa kilomita 20 za barabara inayoelekea Bandari ya Karema, akisisitiza umuhimu wa barabara hiyo katika kufungua fursa za biashara, usafirishaji na kukuza uchumi wa Katavi.

Makamu wa Rais amesisitiza matarajio ya Serikali ni kuona kazi zinakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyowekwa.

Akitoa maelezo, Mkurugenzi wa TANESCO Bw. Lazaro Twange, kuhusu mpango wa kuongeza uwezo wa umeme hadi megawati 80, Twange ameahidi kufikia tarehe 01 Desemba miundombinu ya kuongeza umeme Mpanda itakuwa imekamilika na kutatua Changamoto kubwa ya upungufu wa umeme iliyopo sasa mkoani Katavi.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Hoza Mrindoko, alimpongeza Makamu wa Rais kwa kuwasili mkoani humo na kumwomba kufikisha salamu za shukrani kwa Rais kutokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali uliofanyika Katavi, akieleza kuwa zaidi ya shilingi trilioni 1.4 zimeelekezwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za wananchi na kukuza uchumi wa mkoa huo.

Katika mapokezi hayo, Makamu wa Rais ameambatana na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso, na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Hoza Mrindoko, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mpanda, Mhe. Charles Venas Philipo, viongozi wa Chama na Serikali pamoja na wananchi waliojitokeza kumpokea.

Makamu wa Rais amewasali mkoani Katavi akiwa njiani kuelekea Sumbawanga mkoani Rukwa kumwakilisha Rais katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2026