Uaminifu na uvumilivu vimetajwa kuwa ni mtaji muhimu kwa vijana wanaotafuta mafanikio katika biashara, kilimo na ubunifu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wadau walioshiriki kongamano la vijana lililofanyika katika ukumbi wa Nazareti Sumbawanga mkoani Rukwa wamewataka vijana kuacha kutaka mafanikio ya haraka na badala yake kujenga misingi imara ya nidhamu, uadilifu na kujituma kuelekea mafanikio hayo.
Oralph Mhema Mkurugenzi Mkuu wa Muhema Agro Chemical Ltd amesema, kampuni yake imewezesha zaidi ya vijana 300 kushiriki katika biashara ya usambazaji wa pembejeo za kilimo hususan mbolea kwa takribani miaka 10 na kupelekea mzunguko wa pembejeo unaozidi tani 80,000, zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 100, huku akisisitiza kuwa uaminifu ni mtaji wa kwanza unaojenga imani kwa wawekezaji na kufungua fursa kwa vijana.
Kwa upande wake, David Davis, mwanzilishi wa kampuni ya Cuttoff inayojihusisha na urejelezaji wa taka, amesema ubunifu, uvumilivu na kujiendeleza kwa kuongeza ujuzi vimemsaidia kuendeleza wazo alilolipata akiwa shuleni.
Amewahimiza vijana kubaini changamoto katika jamii zao na kuzitumia kama fursa za kuanzisha biashara, ikiwemo urejelezaji wa taka na uzalishaji wa mbolea.
Mahmoud Mohamed, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Sumbawanga, amesema, baadhi ya vijana hukwamishwa na haraka ya kutaka kutimiza ndoto zao bila kufuata taratibu zinazohitajika.
Amesisitiza kuwa, uaminifu ni msingi wa kujenga mahusiano na mitandao yenye manufaa katika biashara, kilimo na ajira, huku akiwataka vijana kuwekeza katika ujuzi na kuthubutu kutumia fursa zilizopo kwa busara.
Naye Kelvin Steven, mshiriki wa kongamano kutoka Maswa, mkoani Simiyu, amesisitiza umuhimu wa kuunga mkono bunifu za vijana katika sekta ya kilimo na bidhaa zinazozalishwa nchini ili kukuza uchumi na kutatua changamoto za jamii.

