Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia Masuala yaAfrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya (Mb), ametoa wito wa kuimarishwa kwa Uangalizi wa uchaguzi unaozingatia weledi, usio na upendeleo na unaozingatia ushahidi ili kuimarisha demokrasia, amani na utulivu barani Afrika.
Mheshimiwa Millya ametoa wito huo Oktoba 11, 2026, wakati wa ufunguzi wa pamoja wa mafunzo ya rejea ya Umoja wa Afrika (AU) kwa wataalamu wa timu kuu na timu saidizi pamoja na waangalizi wa muda mfupi wa uchaguzi wanawake na vijana, yanayofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema mafunzo hayo ni uwekezaji katika demokrasia ya Afrika, kusisitiza kuwa waangalizi wa uchaguzi wanapaswa kuzingatia uadilifu, uhuru na weledi, huku wakitegemea ukweli na ushahidi wa kuaminika katika tathmini zao wanazotoa.
Amebainisha kuwa teknolojia mpya, akili unde na mitandao ya kijamii vinaendelea kubadilisha michakato ya uchaguzi, huku taarifa potofu na za kupotosha pamoja na mgawanyiko wa kisiasa vikiibua changamoto zinazohitaji kuboreshwa kwa ujuzi na mbinu za uangalizi wa uchaguzi.
Amesisitiza umuhimu wa kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika utawala wa kidemokrasia, akieleza kuwa mpango wa AU ni hatua muhimu katika kujenga kundi la waangalizi wa uchaguzi la Kiafrika lenye uwakilishi mpana na shirikishi zaidi.
Mheshimiwa Millya pia amesisitiza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendeleza ushiriki wa wanawake na vijana katika mchakato wa kuunganisha Afrika, amani na usalama, pamoja na biashara kupitia Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).
Ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono utawala bora wa kidemokrasia na ushirikiano wa Afrika, nakuwasihi washiriki wa mafunzo hayo kutumia maarifa watakayoyapata kuendeleza michakato ya uchaguzi yenye amani, kuaminika na shirikishi katika bara zima la Afrika.

