Na WMJJWM- Arusha
Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Vickness Mayao, ametoa wito kwa wadau kutoka katika Taasisi za Serikali, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, sekta binafsi na jamii kuunganisha nguvu ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kutatua changamoto zinazoikabili Shule ya Sekondari Losinoni, iliyopo mkoani Arusha.
Akizungumza katika mahafali ya Kidato cha Nne ya shule hiyo ya Kata, Mayao amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora, mazingira salama na fursa za kutimiza ndoto zao.
Amebainisha kuwa, maendeleo ya shule hiyo yanahitaji uwekezaji wa pamoja katika miundombinu na huduma muhimu zinazochochea ufaulu na ustawi wa wanafunzi.
Mayao pia ametoa pongezi kwa walimu, wanafunzi, wazazi, walezi, uongozi wa shule, Serikali na jamii kwa mchango wao katika kufanikisha maendeleo hayo. Hata hivyo, amehimiza wadau kutotosheka na mafanikio yaliyopatikana, bali kuyaona kama chachu ya kuweka malengo makubwa zaidi ya kitaaluma na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani yao.
Mayao amesisitiza kuwa uwekezaji katika elimu ya vijana haupaswi kuishia kwenye madarasa na ufundishaji pekee, bali unapaswa kujumuisha mazingira yanayowawezesha kujenga maarifa, ujuzi, nidhamu, maadili, ubunifu na uzalendo.
“Shule iliyoanzishwa kwa ushirikiano wa Serikali na jamii itaendelea kuwa chachu ya maendeleo iwapo wadau wataunganisha nguvu kuhakikisha kila mwanafunzi anapata mazingira bora ya kujifunzia na nafasi ya kufikia malengo yake” amesema Mayao
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Losinoni Obedi Mollel amesema shule hiyo imepiga hatua katika taaluma, ikiwemo kufanikiwa kuondoa matokeo ya Daraja Sifuri (Division Zero) katika matokeo ya Kidato cha Nne na Kidato cha Pili kwa mwaka 2025. Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za walimu katika ufundishaji, bidii ya wanafunzi katika kujifunza na ushirikiano wa wazazi pamoja na uongozi wa shule katika kusimamia maendeleo ya kitaaluma.
Nao wadau wa maendeleo yakiwemo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wameahidi kushirikiana na Serikali, Halmashauri ya Arusha na jamii ya Losinoni katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili shule zikiwemo patikanaji wa maji ya uhakika na ujenzi wa bweni la wavulana ili kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shuleni na kuimarisha usalama, mahudhurio pamoja na muda wa kujisomea.

