Na Jacqueline Mrisho – MAELEZO
Chama cha Maafisa Uhusiano na Mawasiliano Tanzania (PRST), kikiongozwa na Rais wa Chama hicho, Bi. Annastazia Rugaba, kimetembelea Mji wa Serikali uliopo Mtumba pamoja na miradi ya maji inayotekelezwa katika eneo la Buigiri jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya ratiba ya mkutano wa PRST uliofanyika jijini Dodoma kuanzia Oktoba 8 hadi 10, 2026.
Miradi hiyo inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), inalenga kuhakikisha upatikanaji wa huduma za maji safi na ufanisi katika ukusanyaji na usafirishaji wa maji taka katika Mji wa Serikali.
Taarifa iliyotolewa na Msimamizi wa miradi hiyo, Mhandisi Severine Mkenda wakati wa ziara hiyo imeeleza kuwa, miradi hiyo inatekelezwa kwa gharama ya jumla ya shilingi bilioni 88, ikihusisha usambazaji wa maji safi, ukusanyaji na usafirishaji wa maji taka pamoja na uchakataji wa maji hayo kwa matumizi ya umwagiliaji.
Mradi wa kusambaza maji safi katika Mji wa Serikali, Mtumba unahusisha ujenzi wa mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita 59, huku mradi wa ukusanyaji wa maji taka ukihusisha mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita 40.
Aidha, maji taka yatakayokusanywa katika Mji wa Serikali uliopo Mtumba yatasafirishwa hadi Buigiri kupitia mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita 15. Mradi huo utakapokamilika, maji hayo yatachakatwa na kutumika kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji, hatua inayolenga kuongeza matumizi endelevu ya rasilimali za maji.
Kwa upande wake, Rais wa Chama hicho, Annastazia Rugaba, ametoa wito kwa vyuo vinavyotoa mafunzo ya uhandisi katika ngazi mbalimbali, kuanzia cheti, diploma hadi shahada, kushirikiana na DUWASA kwa kuwaruhusu wanafunzi wao kutembelea miradi ya maji na majitaka ili kupata mafunzo ya vitendo.
Ziara hiyo imefanyika wakati PRST ikitimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, ambapo maadhimisho hayo yamefanyika sambamba na Uchaguzi Mkuu wa viongozi wa Chama hicho pamoja na utoaji wa Tuzo za Umahiri katika Mawasiliano na Uhusiano nchini.
Kupitia ziara hiyo, wanachama wa PRST wamepata fursa ya kujionea utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maji katika Mji wa Serikali na kuelewa hatua zinazochukuliwa katika kuboresha huduma za maji safi, usimamizi wa maji taka na matumizi ya maji yaliyosindikwa kwa shughuli za uzalishaji.

