SASA KUHAKIKI MATANKI 60 KWA SIKU

Kituo cha Uhakiki wa Vipimo cha Misugusugu, kilichopo Kibaha mkoani Pwani, kimeongeza uwezo wa kuhakiki matanki ya magari yanayosafirisha mafuta kutoka matanki nane hadi 60 kwa siku, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wafanyabiashara na wasafirishaji.

 

Meneja wa kituo hicho, Mrisho Mandari, amesema kituo hicho kina jukumu la kuhakiki matanki ya magari yanayosafirisha mafuta ya petroli na dizeli kutoka Tanzania na nchi jirani, zikiwemo Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Burundi.

 

Amesema awali huduma hizo zilitolewa katika kituo cha Ilala, ambacho kilikuwa na uwezo wa kuhakiki matanki manane kwa siku. Hata hivyo, Serikali ilijenga kituo cha Misugusugu ili kuongeza uwezo wa kutoa huduma na kupunguza muda wa kusubiri kwa wateja.

 

Mandari amesema kuwa kwa sasa kituo hicho kina uwezo wa kuhakiki matanki 60 kwa siku, jambo linalowawezesha wasafirishaji kutoka mikoa mbalimbali kupata huduma kwa urahisi na kuendelea na shughuli zao za usafirishaji.

 

Kwa upande wake, Raymond George kutoka Kampuni ya Abood Morogoro amesema ameridhishwa na huduma alizopata kituoni hapo baada ya kufika asubuhi na kukamilisha zoezi la uhakiki siku hiyo hiyo. Amewahimiza wasafirishaji wengine kutumia kituo hicho ili kurahisisha shughuli zao.

 

Naye Anthony Mulenga kutoka Zambia, anayefanya kazi katika Kampuni ya Latitude, amesema kampuni yao hupeleka magari yake Tanzania kwa ajili ya uhakiki wa vipimo. Ameeleza kuwa wamekuwa wakipata huduma nzuri na kwamba madereva wao hawajawasilisha malalamiko kuhusu huduma zinazotolewa kituoni hapo.

Baadhi ya wateja wengine wameeleza kuridhishwa na muda unaotumika kukamilisha uhakiki, wakisema hurudi kituoni hapo vyeti vyao vya uhakiki vinapokaribia kuisha muda wake ili kutekeleza taratibu zinazohitajika na kuendelea na shughuli za usafirishaji.