Na Mwandishi wetu, Simanjiro

MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Manyara, Peter Toima, amempongeza mdau wa maendeleo wa Mkoa huo Taiko Kulunju Ole Tipa kwa namna anavyotoa misaada kwa makundi mbalimbali ya kijamii.

Toima ameeleza hayo kwenye mahafali ya shule ya sekondari Emboreet ya Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki James Ole Millya.

Amesema Taiko ni kijana mwenye maono anayesaidia jamii inayomzunguka hivyo aungwe mkono kwani ni msaada mkubwa kwa makundi mbalimbali.

“Mdau wa maendeleo Taiko amekuwa akichangia maendeleo kwa watu mbalimbali, nampongeza kwa hilo aendelee na moyo huo huo wa kusaidia jamii,” amesema Toima.

Diwani wa Kata ya Loiborsiret, Ezekiel Lesenga (Maridadi) amesema anampongeza mdau wa maendeleo Taiko ambaye amekuwa akijitolea kwa jamii kila wakati anapohitajika.

Mardadi amesema mdau huyo wa maendeleo Taiko amesaidia mtu mmoja mmoja, vikundi vya kijamii wakiwemo wanawake kwa kuwanunulia mashine ya kusaga nafaka na kukoboa.

Diwani wa Kata ya Komolo Saning’o Somii amesema mdau wa maendeleo Taiko anapaswa kuungwa mkono kutokana na kusaidia jamii bila kutaka kugombea nafasi yoyote.

“Taiko namfananisha na mtu mmoja kwenye Kata yangu anaitwa Noah Mambush Simbaa ambaye amejenga madaraka na nyumba ya walimu,” amesema Somii.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya ambaye pia ni Mbunge wa Simanjiro, amempongeza Taiko kwa kuwa msaada mkubwa kwa jamii.

Ole Millya amesema Taiko ni kijana mkarimu kwa jamii na hata yeye alipokuwa katika ziara yake kwenye Kata ya Loiborsiret, alilala kwenye boma yao.