Afisa masoko wa kiwanda cha MCCCO David Haule akitoa elimu kuhusu matumizi ya mkaa unaotokana na Pumba za Kahawa kwa baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Mbinga.
………..
Na Mwandishi wetu.
Mbinga
KIWANDA cha kukoboa kahawa cha Mbinga Coffee Curing Company(MCCCO) kinachomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na wakulima wa kahawa,kimeanza kuzalisha mkaa mbadala wa kupikia kwa kutumia pumba za kahawa.
Uzalishaji huo ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan ya uhifadhi wa mazingira,na kuhamasisha jamii kutumia nishati safi ya kupikia.
Meneja uzalishaji wa kiwanda hicho Rabia Ulomi alisema,kama wadau wakubwa wa mazingira wameipa kipaumbele ajenda hiyo kwa kuwa inakwenda kuokoa kiasi kikubwa cha miti ambayo ilikuwa inateketea kwa ajili ya shughuli za kibinadamu.
“Kwa miaka mingi pumba za kahawa zilikuwa zinachomwa moto kama sehemu ya kutunza mazingira,lakini njia hiyo haikuwa salama sana kwani kulikuwa na uharibifu wa mazingira, hivyo kuanza kutengeneza mkaa itasaidia kuhifadhi mazingira na kupunguza ukataji miti ovyo ili kupata kuni na mkaa na kuongeza thamani ya zao la kahawa ”alisema Ulomi.
Ulomi alisema kuwa,kiwanda hicho kinakoboa zaidi ya tani 12,000 za kahawa ghafi kwa mwaka,hivyo kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 700 hadi 800 za mkaa wa kupikia,hivyo itapunguza kiwango kikubwa ukataji miti.
Afisa masoko wa kiwanda hicho David Haule alisema,mkaa unaozalishwa na kiwanda hicho unajulikana kama Mkaa Ember ambao una uwezo wa kukaa na moto kwa muda mrefu,hauna moshi kama ilivyo mkaa unaozalishwa na makampuni mengine na bei ni Sh.500 kwa kilogramu moja.
Alisema,tangu walipoanza uzalishaji mwitikio ni mkubwa wa watu binafsi kwenda kununua kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na wafanyabiasha hasa mama na baba lishe ambao wanajivunia uwepo wa nishati hiyo ambayo imesaidia kuwapunguzia gharama za maisha.
Alisema,kwa sasa wanaendelea kufanya tafiti ya teknolojia bora na rafiki ya uzalishaji wa mkaa mbadala ili uzalishaji utakapokuwa mkubwa uweze kuleta tija kwa watanzania na kuongeza mapato ya kiwanda.
Mkuu wa shule ya sekondari Nyoni Neema Msomi alisema,mkaa huo utasaidia kupunguza gharama ya kununua kuni na mkaa kwa ajili ya kupika chakula cha wanafunzi na kuepusha madhara ya kiafya kwa wapishi kwa kuvuta moshi.
Msomi,ameshauri kiwanda hicho kuzalisha mkaa kwa wingi ili taasisi ambazo zina mkusanyiko mkubwa wa watu hasa shule ziweze kunufaika na mradi huo.
Alisema,kabla Serikali haijazindua matumizi ya nishati safi ya kupikia walikuwa wanatumia zaidi ya Sh.300,000 hadi 400,000 kununua kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia ambayo ni gharama kubwa.
