Rasi wa Chuo Kikuu cha Mkwawa Profesa Method Samuel

……….
NA DENIS MLOWE, IRINGA
CHUO Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kimeahidi kushiriki katika mbio za Kitonga Marathon zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 31, 2026, wilayani Kilolo mkoani Iringa, kikieleza kuwa zitakuwa fursa ya kuhamasisha afya, kutangaza taasisi na kuimarisha mahusiano na jamii.
Ahadi hiyo imetolewa na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Method Samuel, baada ya kupokea ugeni wa waratibu wa Kitonga Marathon waliotembelea chuo hicho kwa ajili ya kuhamasisha ushiriki wa taasisi hiyo katika mbio hizo.
Profesa Samuel amesema chuo kinapongeza juhudi za waandaaji kuja na wazo la kuandaa mbio hizo, akieleza kuwa ni ubunifu unaoweza kuleta manufaa mbalimbali kwa jamii, ikiwemo kuimarisha afya za washiriki na kutangaza vivutio na fursa zilizopo Kilolo.
Amesema ushiriki wa chuo hicho pia utasaidia kutangaza shughuli zake kwa umma, ili watu wengi zaidi wafahamu huduma na mchango wake katika jamii, sambamba na kutekeleza maelekezo ya Serikali kuhusu kuimarisha uhusiano kati ya taasisi na wananchi.
Ameongeza kuwa mbio hizo zitakuwa jukwaa la kujenga mahusiano mazuri kati ya chuo hicho na wadau wa Wilaya ya Kilolo, ambao ni sehemu ya jamii inayohudumiwa na taasisi hiyo.
Profesa Samuel amesema ushiriki huo utatoa fursa kwa wafanyakazi wa chuo kukutana na watu kutoka maeneo mbalimbali, kujenga mitandao ya mawasiliano na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala yenye manufaa kwa maendeleo ya jamii.
Amesema chuo kimejipanga kushiriki kikamilifu na kuunga mkono juhudi za waandaaji katika maandalizi ya mbio hizo, akihimiza wadau wengine kuunga mkono tukio hilo.
Wakati huohuo, mtangazaji maarufu nchini, Maulid Kitenge, amethibitisha kushiriki katika Kitonga Marathon kupitia ujumbe uliosambazwa kwenye ukurasa wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Siwema H. Jumaa.
Kitenge, ambaye pia ametaja ushiriki wa kundi la Crown Jogging la jijini Dar es Salaam, amewahimiza wananchi kujisajili mapema ili kushiriki katika mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu, katika eneo la Mlima Kitonga, wilayani Kilolo.
Amesema maandalizi ya kushiriki yako tayari, huku akitoa wito kwa wananchi na wadau wa michezo kujitokeza kwa wingi kuunga mkono tukio hilo.
Kitonga Marathon inalenga kutumia michezo kama jukwaa la kuhamasisha afya, kutangaza utalii na fursa za uwekezaji, pamoja na kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kuitangaza Wilaya ya Kilolo kwa watu kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Siwema H. Jumaa alisema mbio hizo zitahusisha mbio za barabarani za kilomita tano, 10 na 21, pamoja na trail run ya Mlima Kitonga, ambayo itafungua fursa kwa wananchi na wageni kushiriki shughuli za hiking na utalii wa asili katika eneo hilo.
Mkurugenzi Siwema alisema waandaaji wanatarajia kupata washiriki wasiopungua 800, huku usajili ukiendelea.
Alisema washiriki wa mbio za kilomita tano, 10 na 21 watalipia Sh50,000, huku watakaoshiriki mbio za kupanda Mlima Kitonga wakilipa Sh70,000 na kupata T-shirt, begi, medali na namba ya mshiriki.
Katika mbio za kilomita 21, mshindi wa kwanza atapata Sh1 milioni, wa pili Sh600,000 na wa tatu Sh400,000 kwa upande wa kilomita 10, washindi watatu wa kwanza kwa wanawake na wanaume watapata Sh500,000, Sh300,000 na Sh200,000 mtawalia
