Dar es Salaam-Tanzania, 9 Oktoba 2026: Kombe la Ligi Kuu ya Uingereza limewasili Tanzania, kwa mara ya kwanza, likiashiria kuanza kwa ziara yake ya Afrika Mashariki. Kombe hilo limeletwa na bia ya Guinness, ambayo ni mmoja wa wadhamini wa vinywaji wa Ligi Kuu hiyo kubwa ya soka duniani.
Kuwasili kwa Kombe hilo kunaashiria kuanza kwa sherehe za siku mbili zitakazounganisha hadhi ya Ligi Kuu ya Uingereza na utamaduni wa soka Tanzania.
Kwa Guinness, kuwasili kwa Kombe hili si suala la kuleta tu moja ya alama zinazotambulika zaidi katika soka duniani, ni kutengeneza tukio ambalo linaunganisha soka la kimataifa na mapenzi, nguvu na utamaduni wa soka la Tanzania.
Kuhusu ujio huo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Serengeti Breweries Dk. Obinna Anyalebechi alisema:
“Ligi Kuu ya Uingereza tayari ina nafasi kubwa katika mioyo na mazungumzo ya mamilioni ya mashabiki wa soka, wakiwemo Watanzania. Kinachofanya tukio hili kuwa tofauti ni kwamba sasa Kombe lenyewe limefika hapa, likikutana na mashabiki mahali ambapo mapenzi yao kwa soka yanaishi. Tunataka kuandaa tukio ambalo lina ladha ya Tanzania na kuipa dunia nafasi ya kuona kinachotokea pale soka la kimataifa linapokutana na nguvu, ubunifu na mapenzi yetu wenyewe kwa mchezo huu.”
Kuwasili kwa Kombe hilo pia kumeingia moja kwa moja kwenye utamaduni mkubwa wa soka nchini, huku mashabiki wa Simba SC na Young Africans (Yanga) wakiwa sehemu ya hamasa hiyo. Klabu hizi mbili ni miongoni mwa makundi makubwa zaidi ya mashabiki nchini, huku wengi wao pia wakifuatilia kwa karibu Ligi Kuu ya Uingereza.
Mkurugenzi wa Masoko na Ubunifu wa Kampuni ya Bia ya Serengeti Henry Esiaba alisema:
“Tanzania ina utamaduni mkubwa sana wa soka, na kulileta Kombe la Ligi Kuu ya Uingereza hapa kumetupa nafasi ya kuona mapenzi hayo kwa karibu. Tanzania ikiwa sehemu ya safari hii ya Afrika Mashariki, tunataka Kombe hili liwe sehemu ya tukio halisi la soka la Tanzania tukio hili liongozwe na mashabiki, simulizi zao na namna wanavyosherehekea ujio wa Kombe hili na mchezo wa soka kwa ujumla.”
Kwa jamii ya soka Tanzania, tukio hili pia linaunganisha utamaduni unaokua wa soka nchini na ulimwengu mpana wa soka la kimataifa.
Mwakilishi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Aaron Nyanda alisema:
“Kuwasili kwa Kombe la Ligi Kuu ya Uingereza kunaonyesha uhusiano mkubwa uliopo kati ya jamii yetu ya soka na soka la kimataifa. Kuanzia hamasa inayozunguka klabu zetu hadi Ligi Kuu ya Uingereza na mashindano ya kimataifa, mashabiki wa Tanzania wanafuatilia soka katika ngazi mbalimbali. Tukio hili linaunganisha mapenzi hayo na kuwapa mashabiki wetu nafasi ya kukutana na soka la kimataifa kwa namna tofauti.”
Umuhimu wa tukio hili unaenda zaidi ya soka, kwa kuunganisha michezo, burudani, utamaduni na vijana, huku Tanzania ikipata nafasi ya kuionyesha dunia mapenzi na utamaduni wake wa soka.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, aliyehudhuria tukio hilo alisema:
“Michezo huwaleta watu pamoja, hutengeneza fursa kwa vijana na kutoa nafasi kwa nchi kuonyesha utamaduni na utambulisho wake. Kwa hiyo, kuwasili kwa Kombe la Ligi Kuu ya Uingereza si tukio kwa mashabiki wa soka pekee, bali pia ni fursa ya kuonyesha nafasi kubwa ambayo michezo inaendelea kuwa nayo katika jamii yetu.”
Baada ya Tanzania, Kombe hilo litaendelea na safari yake nchini Uganda tarehe 11 hadi 13 Oktoba na kumaliza safari yake nchini Kenya.
Ligi Kuu ya Uingereza ni miongoni mwa ligi zinazotoa ushindani mkubwa na soka linalovutia zaidi duniani. Kupitia umaarufu wake duniani, ligi hii pamoja na vilabu vyake huwafikia na kuwahamasisha mashabiki, jamii na washirika mbalimbali nchini Uingereza na maeneo mengine duniani.
Ligi hiyo inawaleta pamoja watu kutoka katika makundi na asili mbalimbali, na ni mashindano yanayolenga kila mtu, kila mahali. Kwa sasa, mashindano haya yanawafikia watazamaji katika kaya milioni 920 katika nchi 189 duniani.

