Afisa Mahusiano wa Benki ya Azania, Tawi la Arusha City , Davis Lisapita wakati akizungumza katika Tamasha la Arusha Artisan Festival linaloendelea katika viwanja vya General Tyre, Njiro jijini Arusha.
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha. Benki ya Azania imewataka wasanii nchini kutumia fursa za huduma za kifedha zinazotolewa na benki hiyo, ikiwemo akaunti za biashara, huduma za malipo pamoja na mikopo, ili kukuza shughuli zao za sanaa na kuzifanya kuwa biashara endelevu.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Afisa Mahusiano wa Benki ya Azania, Tawi la Arusha City , Davis Lisapita wakati akizungumza katika Tamasha la Arusha Artisan Festival linaloendelea katika viwanja vya General Tyre, Njiro jijini Arusha.
Lisapita amesema benki hiyo inawatambua wasanii kama wafanyabiashara wanaotumia vipaji vyao kuzalisha kipato.
“kwa kutambua mchango wa wasanii katika uchumi, Benki ya Azania imeamua kushirikiana nao kwa kuwapatia huduma mbalimbali za kibenki zinazoweza kurahisisha uendeshaji wa biashara zao na kuwawezesha kuzifikisha katika hatua kubwa zaidi.”amesema Lisapita.
Lisapita amesema miongoni mwa huduma zinazopatikana ni akaunti za biashara zenye gharama nafuu, pamoja na huduma za malipo za merchant zinazowawezesha wasanii kupokea malipo kutoka kwa wateja mbalimbali, wakiwemo watalii na wageni wanaotumia kadi za Visa.
Ameongeza kuwa,huduma hizo ni muhimu kwa wasanii wanaouza kazi zao kwa watalii, kwa kuwa zinawapa fursa ya kupokea malipo kwa njia za kielektroniki bila kutegemea fedha taslimu pekee, hivyo kurahisisha biashara zao.
Amefafanua kuwa, benki hiyo inatoa mikopo kwa wasanii wanaokidhi vigezo, ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha kupata mtaji wa kuendeleza shughuli zao, kuongeza uzalishaji na kupanua biashara zinazotokana na vipaji vyao.
Lisapita amesema miongoni mwa vigezo vya msingi kwa msanii anayehitaji mkopo ni kuwa na matumizi ya kawaida ya benki, ikiwemo kuweka fedha, kutoa fedha na kufanya miamala kupitia akaunti ya Azania Bank.
Amefafanua kuwa, msanii pia anatakiwa kuwa na chanzo cha mapato kinachoeleweka, ambapo katika mazingira yao chanzo hicho ni biashara ya sanaa anayofanya, kwa kuwa mapato yanayotokana na biashara hiyo ndiyo yanayoweza kutumika katika marejesho ya mkopo.
Aidha amewataka wasanii kusajili shughuli zao za sanaa kama biashara, na kusema usajili unaweza kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha na kuongeza uhalali wa shughuli zao wanapohitaji kupata mitaji kwa ajili ya kukuza biashara.
Kwa upande wa dhamana, Lisapita amesema mwombaji wa mkopo anatakiwa kuwa na dhamana inayokubalika kwa mujibu wa masharti ya mkopo, ambayo inaweza kuwa mali kama kiwanja kilichofanyiwa maendeleo.
Hata hivyo, amesema wasanii wadogo ambao wanaweza kukosa dhamana ya kutosha wakiwa mmoja mmoja wanaweza kuungana na kuunda vikundi, kisha kuomba mikopo kwa pamoja ili kusaidiana katika kutimiza masharti ya mkopo.
Lisapita amesema mfumo huo unatoa fursa kwa wasanii kubebana na kutumia nguvu ya kikundi katika kupata mitaji, badala ya kila msanii kutegemea uwezo wake binafsi pekee katika kutafuta fedha za kuendeleza biashara.
Aidha amewataka wasanii kutumia huduma za Azania Benki kwani benki hiyo inalenga kutoa huduma zenye gharama nafuu katika maeneo mbalimbali, ikiwemo makato ya akaunti, miamala ya kutuma na kupokea fedha pamoja na riba kwa mikopo, kulingana na bidhaa na masharti husika.
Amesema Azania Benki ni benki ya Tanzania inayomilikiwa kwa kiwango kikubwa na mifuko ya kijamii, ikiwemo PSSSF, NSSF, NHIF na WCF, ambapo benki hiyo inaendelea kuweka huduma zinazolenga kukidhi mahitaji ya Watanzania, huku akiwahakikishia wasanii kuwa benki hiyo iko tayari kushirikiana nao bega kwa bega katika safari ya kukuza biashara zao.
