*********************************
Paris St-Germain (PSG) wametangazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu nchini Ufaransa Ligue1 2019/20 baada ya msimu huo kufutwa kufutia katazo la shughuli zote za michezo nchini humo hadi Septemba 1, 2020.
Hadi serikali inatangaza kusitisha michezo Machi 13 mwaka huu kutokana na janga la coronavirus, PSG walikuwa wakiongoza ligi kwa tofauti ya pointi 12 dhidi ya anayewafuata, huku wakiwa bado na mchezo mmoja mkononi.
Kwa upande wa ligi daraja la kwanza Ligue2, Lorient wametangazwa kuwa mabingwa wakiwa na pointi moja mbele ya Lens, hivyo timu zote mbili zitapanda daraja kuingia Ligue1 huku Amiens na Toulouse zikishuka daraja kwenda Ligue2
“Kunaweza kuwa na rufaa, lakini uamuzi wetu hautabadilika”, amesema Didier Quillot, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (LFP) akiongeza kuwa wamejipa muda hadi Mei 25 kuitaarifu UEFA ni timu zipi zitashiriki michuano ya Ulaya msimu ujao.
Awali, chama cha soka nchini humo kilipanga ligi kurejea Juni 17, lakini mapema wiki hii Waziri Mkuu wa nchi hiyo Edouard Philippe, akatangaza kufutwa kwa msimu.