Benki ya NMB imepeleka ujumbe wa ngazi ya juu London, Uingereza, utakaoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Ruth Zaipuna, kushiriki Tanzania Investment Forum 2026 inayofanyika Oktoba 8, ikiwa na lengo la kuunganisha fursa za uwekezaji nchini na mitaji ya kimataifa. NMB ni Mshirika Mkuu wa Kimkakati katika uandaaji wa jukwaa hilo.
Jukwaa hilo litawakutanisha viongozi wa Serikali, wawekezaji, taasisi za fedha na viongozi wa biashara kujadili uwekezaji katika miundombinu, nishati, viwanda, teknolojia, madini, kilimo na sekta nyingine zenye nafasi kubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Zaipuna amesema Tanzania ina fursa kubwa kwa wawekezaji wa muda mrefu kutokana na soko la watu zaidi ya milioni 65, nafasi yake ya kimkakati katika Afrika Mashariki na Kati pamoja na rasilimali na sekta mbalimbali zinazohitaji mitaji. Amesema NMB iko tayari kuwa kiungo kati ya wawekezaji wa kimataifa na fursa hizo kupitia uwezo wake wa kifedha na uelewa wa soko la ndani.
NMB inaingia katika jukwaa hilo ikiwa na mali za takribani Sh18 trilioni, amana za wateja za karibu Sh13 trilioni na wateja zaidi ya milioni 10. Benki pia ina uzoefu wa masoko ya mitaji ya kimataifa kupitia Hati Fungani ya Jamii, ambayo sehemu yake ya dola milioni 73 iliingizwa katika masoko ya London Stock Exchange.
