…………………………………………………………………..
Nyota wa Filamu wa Bollywood nchini India, Rishi Kapoor, aliyejizolea sifa za kucheza filamu za kimapenzi, amefariki dunia kwa ugonjwa wa saratani akiwa na miaka 67.
Nyota huyo ambaye alijizolea sifa nyingi na mafanikio tangu aingie kwenye fani hiyo mwaka 1973 akicheza filamu yake ya kwanza kama kijana iliyojulikana kwa jina la Bobby, aliendelea kuwa tishio katika nafasi yake hiyo kwa kushiriki filamu nyingine nyingi kwa zaidi ya miongo miwili ya mafanikio.
Rishi Kapoor pia aliwahi kuigizaji alikiwa mtoto mwaka 1970 katika filamu ya Baba yake Raj Kapoor iliyojulikana kama Mera Naam Joker.
Miongoni mwa filamu ambazo amewahi kucheza wakati wa uhai wake kati ya miaka ya 1980 na 90 ni pamoja na Khel Khel Mein, Karz na Chandni na kuja kuwa maarufu katika ulimwengu wa filamu.
Alikuwa ni mwigizaji mwenye ujuzi wa kucheza na baadhi ya nyimbo zake mpaka leo bado ni maarufu kwa sehemu kubwa.
Kapoor katika uigizaji wake wa filamu za mapenzi alivutia mno aliposhirikiana na mwigizaji wa kike wakati huo Neetu Singh ambaye baadaye walihamishia uingizaji huo katika maisha halisi nje ya Bollywood na kuoana mwaka 1980.
Mtoto wao wa kiume Ranbir Kapoor, Kwa sasa ni miongoni mwa waigizaji nyota wa Bollywood.
Rishi Kapoor pia alikuwa na ushirika mzuri kwa mara kadhaa na muigizaji nguli Amitabh Bachchan na mjomba wake Shashi Kapoor.
Mwigizaji huyo alizaliwa huko nchini Pakistan katika mji wa Peshawar na familia yake baadaye ilihamia nchini India mwaka 1947 baada ya nchi hizo kugawanyika.