Mkuu wa Mkoa wa Arusha,CPA Amos Makalla akizungumza kwenye kikao hicho jijini Arusha leo

Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Mcha Hassan Mcha akizungumza katika kikao hicho jijini Arusha leo

Happy Lazaro, Arusha. 

Arusha .Mkuu wa Mkoa wa Arusha,CPA Amos Makalla amesema zaidi ya wajumbe 400 kutoka mataifa 48 wanatarajiwa kuwasili jijini Arusha kuhudhuria Mkutano wa 46 wa Wakuu wa Mamlaka za Mapato wa Jumuiya ya Madola, unaofanyika kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026. 

Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mkutano wa 46 wa mamlaka za kodi jumuiya ya Madola (CATA) utakaofanyika Oktoba 6 jijini Arusha katika Hoteli ya Grand Melia Arusha . 

CPA Makalla ameitumia nafasi hiyo kuipongeza TRA kwa kuaminiwa kuwa mwandaaji na mwenyeji wa mkutano huo, ambapo mgenirasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi. 

CPA Makalla amesema kuwa , maandalizi yamekamilika, huku akihakikisha wageni watapata usalama na mazingira mazuri wakati wote watakapokuwa jijini humo. 

Amesema kaulimbiu ya mkutano huo inalenga matumizi ya teknolojia katika kuboresha ufanisi wa ukusanyaji wa mapato, hivyo Tanzania itapata fursa ya kujifunza mbinu mbalimbali zinazotumiwa na mamlaka za kodi za nchi nyingine. 

CPA Makalla amesema kuwa, mkutano huo utaiwezesha TRA kubadilishana uzoefu kuhusu usimamizi wa kodi, ukusanyaji wa mapato na matumizi ya teknolojia ya uchambuzi wa taarifa pamoja na ubunifu katika utoaji wa huduma kwa walipakodi.

 

Amesema ushiriki wa wataalamu kutoka mataifa mbalimbali utasaidia kujenga uwezo wa wataalamu wa Tanzania na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya kodi, hasa kutokana na kuongezeka kwa biashara zinazovuka mipaka.

 

Ameongeza kuwa Tanzania itapata nafasi ya kujifunza mifumo ya kiteknolojia inayotumika katika mamlaka nyingine za kodi na kutathmini namna inavyoweza kuendana na mazingira na mahitaji ya nchi. 

CPA Makalla amewataka wananchi na watoa huduma Arusha kutumia fursa hiyo kuwahudumia wageni kwa ukarimu na upendo, akisema wajumbe hao watatumia hoteli, usafiri na huduma mbalimbali wakati wa kukaa jijini humo. 

Amesema huduma bora inaweza kuwafanya wageni hao kurejea Tanzania kwa shughuli nyingine, ikiwemo utalii na uwekezaji, hivyo wananchi wanapaswa kutumia mkutano huo kutangaza utamaduni wa Watanzania wa ukarimu. 

CPA Makalla ameongeza kuwa mwenyeji wa mkutano huo pia ni fursa ya kuitangaza Tanzania kimataifa na kuonyesha uwezo wa nchi kuandaa mikutano mikubwa, huku Arusha ikipata nafasi ya kutangaza vivutio vyake, ikiwemo Serengeti, Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro.

 

CPA Makalla ameitumia nafasi hiyo kuipongeza TRA kwa kuaminiwa kuwa mwandaaji na mwenyeji wa mkutano huo, huku akitangazaMakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ndiye atakayekuwa mgeni rasmi na anatarajiwa kuufungua mkutano huo Oktoba 6 jijini Arusha. 

Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Mcha Hassan Mcha amesema mkutano huo utajadili pia masuala ya kodi za kimataifa, ikiwemo namna ya kushughulikia kampuni zinazofanya biashara katika nchi zaidi ya moja na kuwa na matawi au mitandao ya biashara katika mataifa mbalimbali. 

Amesema wataalamu watabadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya kutoza kodi kwa kampuni za kimataifa zinazofanya shughuli katika nchi tofauti, huku wakizingatia mifumo na taratibu zinazokubalika kimataifa. 

Mcha Hassan Mcha ameongeza kuwa huduma kwa walipakodi ni miongoni mwa maeneo yatakayojadiliwa, kwa kuwa viwango vya huduma hutofautiana kati ya nchi, huku TRA ikilenga kujifunza ili kufikia viwango vya kimataifa katika kuwahudumia walipakodi nchini. 

Aidha, amesema mkutano huo utajadili uchumi wa kidijitali na biashara zinazofanyika kupitia mitandao, pamoja na kubadilishana ujuzi na uzoefu utakaosaidia mamlaka za kodi kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya teknolojia.