Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Septemba 27, 2026
BAADHI ya wananchi na wawekezaji katika eneo la Zegereni, Kibaha, wameiomba Serikali kujenga kwa kiwango cha lami barabara yenye urefu wa takribani kilometa 2 inayounganisha eneo hilo na viwanda, wakieleza kuwa hatua hiyo itakuwa suluhisho la kudumu la changamoto ya miundombinu inayojitokeza zaidi wakati wa mvua.
Wamesema ujenzi huo utaendana na kasi ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika eneo hilo, ambalo limeendelea kuwa na uwepo wa viwanda na kuongeza mahitaji ya miundombinu bora ya usafirishaji.
Meneja wa Kinglion Investment Company, Kelvin Richard Boya, alisema ubovu wa barabara hiyo huathiri shughuli za uzalishaji, hasa wakati wa mvua, kutokana na magari makubwa kushindwa kupita kwa urahisi na hivyo kuchelewesha uingizaji wa malighafi pamoja na usafirishaji wa bidhaa.
Alisema hali hiyo wakati mwingine husababisha uzalishaji kusimama kwa muda na kuviingiza viwanda katika gharama na hasara zisizotarajiwa.
“Kusimama kwa uzalishaji viwandani kutokana na ubovu wa barabara, magari makubwa hushindwa kupita kufikisha malighafi au kusafirisha bidhaa zilizotengenezwa, Hali hii inasababisha viwanda kusitisha uzalishaji kwa muda na kupata hasara kubwa,” alisema Kelvin.
Kwa upande wake, dereva wa lori, Hamis Hassan, alisema madereva wa malori na magari ya makontena wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kukwama kwenye matope wakati wa mvua, hali inayochelewesha mizigo kufika sokoni na kuongeza gharama za uendeshaji.
Akizungumza kutoka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Kibaha, Colin Mwasheni, alisema barabara hiyo inayotambulika kama Zegereni Industry 5 ipo katika mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami ili kutoa huduma ya kudumu kwa shughuli za viwanda na wananchi wanaoitumia.
Mwasheni alieleza kinachohitajika kwa sasa ni upatikanaji wa fedha ili kuwezesha kuanza kwa utekelezaji wa ujenzi huo.
Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, alisema barabara hiyo ni muhimu kwa kuwa inahudumia viwanda tisa pamoja na wananchi, hivyo uboreshaji wake unaendana na azma ya kukuza uchumi kupitia uwekezaji na viwanda.
Alifafanua kuboresha miundombinu inayowaunganisha wawekezaji na masoko kutasaidia kuongeza shughuli za uzalishaji, mapato na fursa za ajira.
Dkt. Mawazo alielezea, Manispaa ya Kibaha inaendelea kuweka mipango na mikakati ya kuboresha mazingira ya uwekezaji, ikiwa ni sehemu ya kwenda sambamba na juhudi za Serikali katika kukuza sekta ya viwanda na uwekezaji nchini.

