Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye Ulemavu), Dk Jim Yonazi, akizungumza kwenye kongamano hilo

……….
Na Happy Lazaro, Arusha.
Serikali imesisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa ufuatiliaji, tathmini na matumizi ya ushahidi katika kufanya maamuzi ya maendeleo nchini, ikieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kutambua changamoto mapema, kuchukua hatua kwa wakati, kujifunza kutokana na utekelezaji na kuboresha huduma kwa wananchi.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Naibu spika wa bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Daniel Sillo kwa niaba ya Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba wakati akifungua kongamano la tano la kitaifa la wiki ya ufuatiliaji na tathmini na ujifunzaji (MEL) linaloendelea katika hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha .
Sillo amesema kuwa ufuatiliaji na tathmini si suala la kukusanya na kuchambua takwimu pekee, bali ni chombo muhimu cha menejimenti kinachosaidia kupima utekelezaji wa malengo, kubaini changamoto na kuchukua hatua kabla hazijaathiri matokeo yaliyokusudiwa.
“Serikali imesema viongozi wanapaswa kutumia taarifa za ufuatiliaji na tathmini katika maamuzi ya kila siku badala ya kusubiri mwisho wa mwaka kubaini mapungufu.”amesema Sillo.
“Serikali imekuwa ikiandaa wataalamu katika taasisi mbalimbali kupitia M&E Champions, huku vijana wanaochipukia katika taaluma hiyo kupitia Tanzania Young and Emerging Evaluators wakitakiwa kuwa chachu ya mabadiliko.”amesema Sillo.
Ameongeza kuwa, ufuatiliaji na tathmini unapaswa kuwa jukumu linaloshirikisha idara na vitengo mbalimbali ndani ya taasisi, si kubaki kwa kitengo kimoja pekee.
Aidha Sillo amesisitiza umuhimu wa tathmini jumuishi inayowashirikisha wanawake, vijana, watu wenye ulemavu, wazee na makundi mengine yenye mahitaji maalum.
“ushahidi unaotumika katika maamuzi haupaswi kuishia kwenye takwimu, bali unapaswa kuonesha hali halisi ya wananchi, kusikiliza sauti zao na kubaini kama maendeleo yanawafikia walengwa kwa usawa.”amesema Sillo.
Aidha katika eneo la teknolojia, amesisitiza umuhimu wa kujenga mifumo ya kidijitali inayoweza kuzungumza na kubadilishana taarifa, kwa kuzingatia dhana ya “One Government, One Results Language.”
Amefafanua zaidi kuwa, Teknolojia, akili mnemba, mifumo ya taarifa za kijiografia, ukusanyaji wa taarifa kwa njia za simu na majukwaa ya wazi ya data ni nyenzo muhimu katika kuboresha ufuatiliaji na tathmini na kuwezesha viongozi kupata taarifa kwa wakati.
“Serikali itaendelea kushirikiana na (Tan EA) vyuo vikuu na taasisi za utafiti katika kuendeleza tafiti, ubunifu, viwango vya tathmini na kujenga uwezo wa wataalamu.”amesema Sillo.
Sillo ameongeza kuwa,kuna umuhimu wa kujenga taaluma inayotambulika kimataifa huku ikizingatia mazingira ya Afrika, ikiwemo kuendeleza mbinu na viwango vya tathmini vinavyotokana na uzoefu wa Afrika, maarufu kama “Made in Africa Methods and Standards in Evaluations.”
Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye Ulemavu), Dk Jim Yonazi, amesema Serikali ikiwa katika awamu ya utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano, inahitaji ushahidi wa matokeo ya mipango yake kwa wananchi.
“Kwa sasa tupo katika awamu ya utekelezaji, siyo awamu ya mipango. Serikali haihitaji tu taarifa zinazoonyesha fedha zilizotumika au miradi iliyojengwa. Inahitaji ushahidi unaoonyesha maisha ya wananchi yamebadilikaje, kwa gharama gani na ndani ya kipindi gani,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa idara ya ufuatiliaji tathmini na ujifunzaji Tanzania ,Sakina Mwinyimkuu amesema ufuatiliaji na tathmini si jukumu la taasisi moja pekee, bali ni wajibu wa pamoja wa wadau wote wa maendeleo katika kuhakikisha utekelezaji wa afua mbalimbali unaleta matokeo chanya kwa jamii.
Amesema mikutano na makongamano ya wadau ni muhimu kwa kujifunza kwa pamoja na kubadilishana uzoefu na maarifa yanayoweza kuboresha utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo.
Sakina amesisitiza kuwa ushirikiano huo unapaswa kuelekezwa katika kuhakikisha wananchi wanapata manufaa halisi kutokana na afua zinazotekelezwa.
Amesema washiriki wanapaswa kutumia kongamano hilo kama fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kutoa mawazo yatakayosaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji na ufuatiliaji wa miradi na programu za maendeleo.
Amefafanua kuwa, jukumu la ufuatiliaji na tathmini linahitaji ushiriki mpana wa wadau ili kuhakikisha mipango ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta manufaa kwa jamii, akiwataka washiriki kushiriki kikamilifu katika majadiliano na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha utekelezaji wa afua mbalimbali.
Naye Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TanEA, Almasi Mazigo, ameiomba Serikali kuharakisha jitihada za kuandaa na kukamilisha Sera ya Taifa ya Ufuatiliaji na Tathmini, akisema itasaidia kuweka mfumo madhubuti wa kusimamia na kuendeleza taaluma hiyo nchini.
Mazigo amesema kuna umuhimu pia wa kuangalia uwezekano wa kuanzishwa kwa bodi maalumu itakayokuwa na jukumu la kusimamia taaluma na kazi za ufuatiliaji na tathmini nchini.
Amesema Tanzania ina wataalamu wenye uwezo katika eneo hilo ambao wanapaswa kuendelea kujengewa uwezo ili waweze kutumia taaluma zao kusaidia kuboresha utekelezaji wa mipango na programu za maendeleo.
