Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amevisisitiza Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Tasisi za Umma, Taasisi binafsi na wananchi kwa ujumla kujenga tabia ya kufanya mazoezi ili kujikinga na maradhi mbalimbali ikiwemo maradhi yasiyo yakuambukiza.
Ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi katika hafla ya ufunguzi wa Michezo ya Majeshi Tanzania ( BAMATA ) 2026, inayofanyika katika Uwanja wa CCM KIRUMBA Jijini Mwanza.
Amesema kufanya mazoezi ya mwili ni jambo muhimu linalosaidia kuimarisha afya ya mwili na akili, utimamu wa mwili pamoja na kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambikiza ikiwemo Sindikizo la damu na kisukari ambayo yamekuwa yakiathiri idadi kubwa ya watu.
Makamu wa Pili wa Rais amesema kila mmoja anapaswa kutambua umuhimu wa kufanya mazoezi katika kujenga utimamu wa akili na mwili, ustawi wa jamii na uzalishaji wenye tija katika kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ya kuwa na Taifa lenye nguvu kazi na afya bora.
Mhe.Hemed amefahamisha kuwa dhamira ya Mashindano ya BAMATA ni kukuza ushindani wa michezo na kubuni michezo mipya mbalimbali itakayoimarisha mshikamano, ushirikiano na mahusiano mema miongoni mwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi kupitia Sekta ya Michezo.
Mhe. Hemed amesema Serikali ya SMT na SMZ zinaendelea kuchukua hatua ya kuboresha miundombinu ya michezo, kuendeleza program za kukuza vipaji, kuimarisha mafunzo ya walimu na makocha wa michezo kwa kuweka mazingira bora yatakayowezesha wanamichezo kufikia viwango vya juuu vya ushindani hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika mashindano makubwa ya AFCON 2027.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amesema Mashindano ya BAMATA 2026 yamesisitiza wanamichezo na wananchi kuendelea kuwa wazalendo wa Taifa lao kwa kudumisha umoja, amani na mshikamano unaochochea kukua kwa uwekezaji, kuongezeka kwa watalii na kupata maendeleo yanayogusa maisha ya wananchi wote kama vile Elimu, Afya, Maji safi na salama, Barabara na mengineyo.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais amebainisha kuwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimekuwa na mchango mkubwa katika suala la ulinzi na usalama wa nchini pamoja na kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji mbalimbali vya michezo ambavyo hulitumia Tamasha la BAMATA katika kujenga uzoefu, kuboresha viwango na kushindana kwa kuzingatia haki, nidhamu na kufuata kanuni na sheria za kuendeshea Mashindano hayo.
Nae Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mheshimiwa Dkt. RHINO SIMEON NYASAHA amesema Mashindano ya BAMMATA huwawezesha wanamichezo Askari kujenga afya, nidhamu, umoja na mshikimano miongoni mwao hasa katika kutimiza majukumu yao ya Ulinzi na usalama wa Raia na mali zao.
Dkt. Rhino amesema katika kutimiza Mkakati wa kuwa na Taifa lenye Amani na mshikamano, vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kushirikiana na Watanzania wote katika kuhakikisha dhamira hio inatekelezwa kwa vitendo ili kuendelea kuwa na Taifa lenye Umoja, Amani na mshikamano wakati wote.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama na Mkuu wa Majeshi ya ulinzi na usalama Tanzania Jenerali JACOB JOHN MKUNDA amekiri kuwa Serikali inathamini mchango unaotolewa na Vyombo vya ulinzi na usalama katika ulinzi wa Taifa na ushiriki wao katika michezo mbalimbali ambayo inawaunganisha wapiganaji wa Majeshi kutoka Kanda mbali mbali Tanzania Bara na Zanzibar.
Jenerali Mkunda ameeleza kuwa michezo ni sehemu ya maandalizi kwa askari inayowaweka tayari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na uweledi mkubwa unaoendelea kuifanya Tanzania kuwa na Amani na utulivu ikiwa ni heshima kubwa kwa Taifa la Tanzania.
Amesema Kamati ya Mashindano ya BAMMATA inajipanga kuimarisha mifumo ya utambuzi, kuboresha vipaji, kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu wakati wa mashindano hata katika kipindi cha maandalizi ya mashindano hayo ili kuyawezesha kufanyika kwa ufanisi, weledi na hadhi ya juu na hatimae kuzalisha wanamichezo wenye uzalendo, nidhamu na utayari wa kulitumikia Taifa.
Mwenyeji wa Mashindano hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza CP SALUM RASHID HAMDUNI amesema ni heshima kubwa kwa Mashindano ya BAMMATA kufanyika katika Mkoa wa mwanza ambayo yanatangaza fursa mbalimbali zilizomo Mkoani humo kupitia utalii wa michezo unaoendelea kufanywa na wageni wanaoingia katika Mkoa huo ambao watahitaji huduma mbalimbali za kiuchumi na kijamii.na kupelekea mzunguko wa fedha kuongezeka na uchumi kuimarika.
CP Hamduni amesema katika kujenga mustakbali mwema wa Taifa ni jukumu la kila mmoja kudumisha Amani ili kujenga jamii jumuishi yenye umoja na mshikamano utakaopelekea kuwa na umahiri wa maendelelo nchini.

