Na. Fullshangwe Blog
MKUU wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewaagiza wafanyabiashara wanaopanga bidhaa zao chini katika barabara za soko la Mbuyuni manispaa ya Moshi kuondoka katika maeneo hayo na kufanya biashara zao ndani ya soko hilo ili kuepuka milipuko ya magonjwa pamoja na uchafuzi wa mazingira.
Babu alitoa kauli hiyo jana wakati wa zoezi la ufanyaji usafi katika soko hilo ambapo alisema kuwa, barabara zimewekwa kwa ajili ya kupita magari na wananchi kupita bila kubugudhiwa.
Alisema kuwa, wafanyabiashara hao ambao wanapanga bidhaa zao chini wanapaswa kwenda kwa viongozi wa soko hilo waweze kuwapangia maeneo ya kufanyia biashara kabla ya serikali haijachukua hatua za kuwaondoa katika maeneo hayo.
“Niwataka muanze kuondoka wenyewe mapema tusije kuja kuwaondoa sisi mkasema tunawaonea serikali imetumia fedha nyingi kujenga masoko haya sasa ni wajibu wenu mkafanye biashara ndani ya masoko haya ambayo yamewekwa miundombinu rafiki ya kuwahudumia” alisema Babu.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa, wafanyabiashara hao wote wakijipanga ndani ya soko hilo wateja watawafuata humo ndani kununua na kuwataka kutekeleza sheria hiyo bila shuruti.

