Na Victor Masangu,Bagamoyo 
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Mhe. CPA. Subira Khamisi Mgalu ameipongeza Mamlaka ya mapato (TRA) Bagamoyo kwa kuweka mipango madhubuti katika suala zima la  ukusanyaji wa mapato.
Mhe.Subira ameyabainisha hayo  wakati alipofanya ziara yake  katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bagamoyo, ambapo amepata fursa ya kukutana   na kufanya mazungumzo na Meneja wa TRA Bagamoyo, Mariam Omari.
Katika mazungumzo hayo, wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu ongezeko la mapato, ukusanyaji wa kodi, kuvuka malengo ya ukusanyaji pamoja na umuhimu wa kuendelea kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kuhusu ulipaji wa kodi.
Mhe. Subira Mgalu ameipongeza TRA Bagamoyo kwa kazi kubwa inayofanyika katika kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unaendelea kuimarika.
 Aidha, ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano na kuhamasisha wananchi katika mikutano yake mbalimbali kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa na Jimbo la Bagamoyo.
Mbunge huyo pia amempongeza Meneja wa TRA Bagamoyo, Mariam Omari, kwa moyo wake wa kujitolea na kusaidia jamii, hususan katika kuchangia uboreshaji wa miundombinu katika Shule ya Msingi Ukuni, ambapo Meneja huyo alialikwa kushiriki katika mahafali ya shule hiyo.
Mhe. Subira ameeleza kuwa juhudi kama hizo za taasisi na watendaji katika kushirikiana na jamii zinapaswa kuungwa mkono, huku akiahidi kuwa balozi wa kudumu wa kuhamasisha ushirikiano kati ya wananchi, taasisi na wadau mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya Bagamoyo.
Mhe. CPA. Subira Khamisi Mgalu amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya viongozi, taasisi na wananchi ni muhimu katika kuongeza uelewa wa ulipaji wa kodi na kuchochea kasi ya  maendeleo