Na Mwandishi Wetu
Mkururugenzi wa shule ya Green Acres ya Mbezi Beach Salasala jijini Dar es Salaam, Jacklline Rushaigo ameelezea namna shule hiyo ilivyoanza kufundisha Teknojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA ili kwenda sanjari na ulimwengu kidijitali.
Akizungumza leo kwenye mahafali ya darasa la saba na shule ya awali ambapo wanafunzi 60 walihitimu elimu ya msingi, Jackline alisema Shule hiyo inatambua umuhimu wa kuzingatia teknolojia za kisasa katika ufundishaji.
“Tumeongeza ubora na ufanisi kwenye TEHAMA, wanafunzi wetu wanajifunza masuala ya akili mnemba wakiwa wadogo hapa shuleni na mambo yanayoendana na uhalisia wa utanzania wetu na dunia ya sasa,” alisema
“Tunawapa taaluma ambayo hata wakiwa nje ya shule wanaweza kufanya vitu mbalimbali vya kujiajiri na kujiingzia kipato, Green Acres tunataka mwanafunzi akimaliza hapa awe na ujuzi wa kutosha kabisa kumwezesha kufanya mambo makubwa,” alisema
Aidha, aliwataka wahitimu wa darasa la saba kuendelea kuwa na nidhamu, bidii na kujituma katika masomo wanapoingia katika hatua nyingine ya elimu.
Alisema mafanikio ya mwanafunzi hayawezi kutenganishwa na ushirikiano wa karibu kati ya shule, walimu, wazazi na walezi
Alieleza kuwa juhudi za pamoja ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora sambamba na malezi yanayojenga maadili, uwajibikaji na kujiamini.
Rushaigo pia aliwashukuru wazazi na walezi kwa kuiamini Green Acres na kushirikiana na uongozi wa shule katika kuwalea na kuwaandaa watoto wao kwa maisha ya baadaye.
Aliwataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata kama msingi wa kufikia malengo yao, huku wakizingatia maadili, kuheshimu wazazi na walimu, na kuwa tayari kujifunza zaidi katika hatua zinazofuata.
Alisema Green Acres itaendelea kuwekeza katika elimu inayolenga kumjenga mwanafunzi kitaaluma, kimalezi na katika nyanja mbalimbali za maisha, ili kuwaandaa vijana wenye uwezo wa kushindana katika dunia inayobadilika kwa kasi.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Edwin Odemba, aliwataka wahitimu kuendelea kuthamini elimu, nidhamu na maadili mema wanapoingia katika hatua nyingine ya masomo yao.
Odemba aliwapongeza wanafunzi kwa kumaliza hatua ya elimu ya msingi na kuwataka kutumia maarifa waliyoyapata shuleni kama msingi wa kujenga maisha yao ya baadaye.
Alisisitiza umuhimu wa wanafunzi kuwa na bidii katika masomo, kuheshimu wazazi, walezi na walimu, pamoja na kutumia muda wao vizuri ili kufikia malengo waliyojiwekea.
Odemba pia aliwataka wazazi kuendelea kushirikiana na walimu katika malezi na elimu ya watoto, akieleza kuwa mafanikio ya mwanafunzi yanahitaji ushirikiano wa familia, shule na jamii kwa ujumla.
Aidha, aliwapongeza walimu na uongozi wa Green Acres kwa mchango wao katika kuwaandaa wanafunzi kitaaluma na kimalezi.
Aliwataka wahitimu kutambua kuwa kumaliza Darasa la Saba si mwisho wa safari yao, bali ni mwanzo wa hatua nyingine muhimu inayohitaji kujituma, kujiamini na kuweka malengo ya muda mrefu.
Odemba aliwahimiza wanafunzi hao kuwa mabalozi wema wa shule yao na kutumia elimu yao kwa manufaa yao, familia zao na jamii.

